By Arushadigial-Dar Es Salaam
Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imekubaliana na pingamizi la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kwamba kizimba maalum kilichotengenezwa kwa ajili ya shahidi wa siri kifanyiwe marekebisho ili majaji waweze kumuona na kutathmini ipasavyo ushahidi wake.
Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiana na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde, baada ya kusikiliza hoja za pande zote. Upande wa Jamhuri ulidai kuwa kizimba hicho kilichotengenezwa kwa mbao (kiboksi) kiliruhusu majaji kumuona shahidi bila tatizo.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Ndunguru amesema kizimba hicho hakikidhi matakwa ya Kanuni ya 3 ya Ulinzi wa Mashahidi, kwani kimejengwa kwa namna inayowazuia majaji kumuona shahidi moja kwa moja.
“Namna kilivyojengewa ni kweli hakikidhi Kanuni ya 3 ya Ulinzi wa Mashahidi na kinafanya majaji washindwe kutathmini ushahidi wake kwa sababu haimuoni. Tunakubaliana na hoja ya mshtakiwa,” amesema Jaji Ndunguru.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa kanuni hiyo, kizimba maalum kinapaswa kuwa sehemu iliyoandaliwa mahususi kumuwezesha shahidi anayeitoa ushahidi kuonekana na jaji au hakimu anayesikiliza shauri.
Hata hivyo, mahakama imekubaliana na pingamizi hilo moja tu kuhusu kizimba, na kuyatupilia mbali pingamizi manne yaliyowasilishwa na Lissu, likiwemo la kupinga matumizi ya Kanuni za Kuficha Mashahidi kwa madai kuwa hazikuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
“Upande wa Jamhuri uliwasilisha nakala ya Gazeti la Serikali lililochapisha kanuni hizo. Mahakama imeona pingamizi la kwanza tu ndilo lenye mashiko; manne yamekataliwa,” amesema Jaji Ndunguru.
Akiwasilisha pingamizi zake, Lissu alisisitiza kuwa shahidi wa siri anapaswa kusimama katika kizimba cha ushahidi kama sheria inavyoelekeza, badala ya kufichwa ndani ya kiboksi kinachozuia kuonekana kwake. Pia alihoji iwapo majaji wanaweza kumuona shahidi huyo, akieleza kuwa sheria inataka shahidi wa siri aonekane na jaji au hakimu, na majina yao yajulikane kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Tundu Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, alitoa kauli zinazodaiwa kuchochea umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, alitamka na kuandika maneno yanayodaiwa kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania akisema miongoni mwa mengine: “Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli..., kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi..., tunaenda kikinukisha..., huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli...”
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu.

0 Comments