DKT. CHARLES MAHERA AWEZESHA SHULE BUTIAMA, MILIONI 66 ZA MFUKO WA JIMBO ZAIMARISHA MIUNDOMBINU YA ELIMU
Na ArushaDigital – Butiama
Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Mahera, amegawa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 66 kwa shule za msingi na sekondari wilayani humo, ikiwa ni sehemu ya matumizi ya Mfuko wa Jimbo yanayolenga kukuza na kuimarisha sekta ya elimu.
Katika hafla ya makabidhiano, shule zilipokea bati, misumari, saruji na mbao kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa madarasa pamoja na miundombinu mingine ya kujifunzia. Hatua hiyo inalenga kuboresha mazingira ya kufundishia kwa walimu na kuongeza tija ya ujifunzaji kwa wanafunzi.
Aidha, shule za sekondari zimepatiwa vitabu vya masomo ya Sanaa na Sayansi vyenye thamani ya shilingi 2,700,000/=, hatua inayotarajiwa kuongeza ubora wa ufundishaji darasani na kuinua viwango vya ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Dkt. Mahera alisema uwekezaji katika elimu ni msingi wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla, akibainisha kuwa Mfuko wa Jimbo utaendelea kutumika kama chachu ya maboresho ya miundombinu na upatikanaji wa rasilimali za kujifunzia.
“Tutaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu bora katika mazingira rafiki na salama,” alisema.
Walimu na wazazi waliohudhuria walieleza matumaini yao kuwa maboresho hayo yatachochea nidhamu, ari ya kujifunza na matokeo bora ya wanafunzi, huku wakimpongeza mbunge huyo kwa kuipa kipaumbele elimu katika ajenda za maendeleo ya Butiama.
...Ends..







0 Comments