AJALI YA MSAFARA WA WAZIRI MKUU YAMUUA MKAZI WA MERERANI
Na Joseph Ngilisho — SIMANJIRO
SIMANJIRO, MANYARA — Mkazi wa Mererani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Justine Abraham Sarakikya maarufu kama Ngumi (51), amefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na gari la msafara wa Waziri Mkuu katika ajali iliyotokea jana majira ya saa mbili usiku.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, ajali hiyo ilitokea karibu na Kituo cha Polisi Mererani wakati marehemu akiwa na pikipiki yake akijaribu kuvuka barabara akielekea nyumbani. Inadaiwa kuwa alidhani msafara wa magari ya Waziri Mkuu uliokuwa ukitokea eneo la Olkesment wilayani Kiteto ulikuwa umepita wote.
Shuhuda wa tukio hilo, Mariamu Hamis, alisema marehemu alikuwa amesimama kando ya barabara akisubiri msafara upite, kisha akaanza kuvuka baada ya kuona magari mengi yameshapita.
“Baada ya magari mengi kupita, marehemu alidhani msafara umeisha. Alipoanza kuvuka barabara, kulikuwa bado na magari matatu nyuma ya msafara. Magari mawili ya kwanza yalifanikiwa kumkwepa, lakini gari la tatu aina ya Land Cruiser lilimgonga bila kusimama na kufariki papo hapo,” alisema Mariamu.
Baadhi ya wananchi waliokuwepo eneo la tukio walikimbilia kumsaidia, lakini jitihada zao hazikuzaa matunda kwani tayari alikuwa amepoteza maisha. Mwili wa marehemu ulipelekwa katika kituo cha afya kilicho karibu kwa taratibu zaidi.
Jitihada za kumpata kamanda wa polisi Mkoani Manyara ili kuzungumzia tukio hilo hazijafanikiwa kutokana na simu zake mbili za umma kutopatikana .
Ziara ya waziri Mkuu ilipangwa kuhitinishwa katika mji wa Mererani jana lakini iliahirishwa kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa wazi japo idadi kubwa ya wananchi walijikusanya kusubiri ujio wake akitokea wilayani Kiteto.
Wakati huo huo Mwili wa Sarakikya maarufu kama Ngumi, aliyefariki kwa kugongwa na gari la msafara wa Waziri Mkuu, unatarajiwa kuzikwa Jumanne.
Taarifa za familia zinasema taratibu zote za mazishi zitafanyika nyumbani kwake Endiamtu, kabla ya mwili kupelekwa shambani kwake Mgutwa kwa maziko.
Ngumi alikuwa mtu maarufu Mererani, mzawa aliyeshiriki kikamilifu shughuli za kijamii na kuhudumu kwa miaka mingi kama Mwenyekiti wa Kitongoji. Pia alikuwa mwanachama hai wa Chama Cha Mapinduzi na mshili wa ukoo wa Sarakikya.
Familia na wakazi wamesema kifo chake kimeacha taharuki kubwa; nyumbani kwake kumefurika waombolezaji kufuatia msiba wa ghafla, huku akiacha pengo kubwa kwa familia na jamii iliyokuwa ikimtegemea katika hatua mbalimbali za maendeleo. Simanzi ni nzito Mererani.
Kifo cha Sarakikya kimeacha huzuni kubwa kwa familia, ndugu na wakazi wa Mererani waliomfahamu kama mtu mchangamfu na mchapakazi katika shughuli zake za kila siku.
Kifo cha Sarakikya kimeacha huzuni kubwa kwa familia, ndugu na wakazi wa Mererani waliomfahamu kama mtu mchangamfu na mchapakazi katika shughuli zake za kila siku.
NB; picha iliyopo haihusiani na tukio la ajali
Ends..


0 Comments