NAIBU WAZIRI AWEKA MSISITIZO EASTRIP, KIKULETWA KUWA KITOVU CHA NISHATI JADIDIFU AFRIKA
Na Joseph Ngilisho – HAI
Naibu waziri wa elimu sayansi na Teknolojia,Wanu Ameir ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi katika Kampasi ya Kikuletwa, Chuo cha Ufundi Arusha, akieleza kuwa mradi huo ni chachu ya mageuzi ya kiuchumi, ajira na ushindani wa kikanda.
Akizungumza mbele ya viongozi wa Serikali, menejimenti ya Chuo, wanafunzi na wananchi wa Wilaya ya Hai, Naibu Waziri amesema uwekezaji unaofanywa kupitia EASTRIP chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan una lengo la kuifanya Kampasi ya Kikuletwa kuwa Kituo cha Umahiri cha Nishati Jadidifu kwa Afrika Mashariki na bara zima.
Alisema kituo hicho ni cha kimkakati kwa kutoa mafunzo ya vitendo katika nishati ya maji, jua, upepo na bioanuwai, sambamba na kuandaa wataalamu watakaohudumia miradi mikubwa ya kitaifa na kimataifa.
Naibu Waziri alibainisha mchango wa mradi katika maandalizi ya nguvu kazi kwa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere, huku ukifungua milango ya ushirikiano wa kikanda kwa kupokea wanafunzi na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kwa ajili ya mafunzo na tafiti. Amesisitiza kuwa hatua hiyo itaongeza hadhi ya Tanzania katika sayansi, teknolojia na uvumbuzi wa nishati safi.
Akiipongeza menejimenti ya Chuo na uongozi wa Wilaya ya Hai, alisema ameridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa mradi, pamoja na mahusiano mazuri kati ya Chuo na wananchi wanaozunguka eneo la mradi. Alisema wananchi wameendelea kunufaika kupitia ajira za muda, huduma za kijamii na fursa za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa mradi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alieleza kufurahishwa na ushiriki wa wakufunzi na wanafunzi katika ujenzi wa mtambo wa kufua umeme, akisisitiza kuwa mbinu hiyo inaongeza ubora wa mafunzo kwa vitendo.
Aidha, amewapongeza wataalamu wazalendo, akiwemo Mhandisi Dkt. Robert Kabudi na wenzake, wahitimu wa Chuo cha Ufundi Arusha, ambao sasa wanashiriki kusimamia miradi mikubwa ya kitaifa.
Kuhusu matumizi ya nishati safi na mabadiliko ya tabianchi, Naibu Waziri amehimiza wanafunzi kuchagua kozi zinazohusiana na nishati jadidifu, akisema ndiko dunia inakoelekea.
Alisema Serikali inaendelea kuboresha mitaala, miundombinu na mazingira ya kujifunzia, hatua iliyosababisha kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi, hususan wasichana, katika kozi za ufundi – jambo alilolitaja kuwa mafanikio makubwa katika kumuinua mtoto wa kike.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuliwezesha Chuo cha Ufundi Arusha kutekeleza kwa vitendo Sera ya Elimu ya mwaka 2014 toleo la 2023, huku akipongeza ushirikiano wa Chuo na viwanda, taasisi za elimu na utafiti ndani na nje ya nchi. Pia aliishukuru Wizara ya Nishati kwa kuunganisha Chuo na International Solar Alliance, hatua itakayowezesha kuanzishwa kwa Kituo Maalum cha Rasilimali ya Nishati ya Jua.
Akihitimisha, Naibu Waziri alisema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha Kampasi ya Kikuletwa inakuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika mafunzo, tafiti na uvumbuzi wa nishati jadidifu, akisisitiza kuwa uwekezaji huo ni msingi wa maendeleo endelevu ya taifa. KUWA KITOVU CHA NISHATI JADIDIFU AFRIKA.
Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Profesa Musa Chacha, alisema utekelezaji wa Mradi wa Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Nishati Jadidifu ni ushahidi wa dhamira ya Serikali katika kuandaa wataalamu wenye ujuzi wa vitendo na kuimarisha mchango wa nishati safi katika maendeleo ya Taifa.
Profesa Chacha alieleza kuwa mradi wa nishati jadidifu unatekelezwa kupitia EASTRIP, unaoshirikisha Tanzania, Kenya na Ethiopia, kwa lengo la kuongeza udahili, kuboresha ubora wa mafunzo ya ufundi stadi na kuimarisha ushirikiano wa kikanda. Kupitia mradi huo, ATC imepatiwa shilingi bilioni 46.7 kuendeleza Kampasi ya Kikuletwa kuwa Kituo cha Umahiri cha Kikanda cha Mafunzo ya Nishati Jadidifu.
Aidha, Profesa Chacha alibainisha mafanikio ya mradi ambapo wanafunzi 3,519 tayari wamepatiwa mafunzo, ikiwemo wanawake na wanafunzi kutoka nchi jirani. Mitaala 27 imetengenezwa, vifaa vya kisasa vya maabara vimenunuliwa, na majengo 11 yamejengwa ikiwemo mabweni, madarasa, karakana na ukumbi wa mihadhara.
Ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa megawati 1.65 unaendelea na unatarajiwa kukamilika Machi 2026. Hata hivyo, Profesa Chacha alitaja barabara ya kufika Kampasi ya Kikuletwa kuwa changamoto kuu, akiomba Serikali kuendelea kuwekeza ili barabara hiyo ikamilike kwa hadhi ya kituo cha kikanda na kimataifa.
Ends...

















0 Comments