VILIO NA SIMANZI ARUMERU: WATOTO WAWILI WAFARIKI KWA KUZAMA KATIKA BWAWA LA HOTELI SAKINA
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Hali ya vilio na simanzi imetanda katika kijiji cha Kimnyaki, wilayani Arumeru, kufuatia vifo vya watoto wawili wa familia moja, Abednego Joachim (13) na Ebenezer Joachim (9), waliopoteza maisha baada ya kuzama kwenye bwawa la kuogelea (swimming pool) katika hoteli moja iliyopo eneo la Sakina, jijini Arusha.
Tukio hilo lililotokea jana January 7,2026 majira ya mchana, limeacha mshtuko mkubwa kwa familia ya marehemu, majirani pamoja na wanakijiji kwa ujumla, huku maswali mazito yakianza kujitokeza kuhusu usalama na udhibiti wa watoto katika maeneo ya burudani.
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, alifika nyumbani kwa familia ya marehemu muda mfupi baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitokea nchini Ujerumani. Akiwa ameguswa sana na tukio hilo, Dkt. Lukumay alishindwa kujizuia na kumwaga machozi, akieleza masikitiko yake makubwa kwa msiba huo mzito.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dkt. Lukumay aliipa pole familia ya marehemu na kuvitaka vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini iwapo kulikuwa na uzembe uliochangia vifo hivyo. Alisisitiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika endapo itabainika sheria na taratibu za usalama zilikiukwa.
“Ni tukio la kusikitisha sana, hasa ikizingatiwa kuwa watoto waliopoteza maisha ni wadogo. Naiomba familia iwe na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu. Hata hivyo, ni wajibu wa vyombo vya usalama kuchunguza kwa umakini kubaini kama kulikuwa na uzembe, na kuchukua hatua stahiki. Wamiliki wa mabwawa ya kuogelea wanapaswa kuhakikisha kunakuwa na wataalamu wa uokoaji na uangalizi wa karibu, hususan kwa watoto,” alisema Dkt. Lukumay.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimnyaki, Samweli Meliyo, alisema tukio hilo limeusikitisha kwa kiwango kikubwa uongozi na wananchi wa kijiji hicho. Alieleza kuwa alipata taarifa za vifo vya watoto hao majira ya saa tisa alasiri, baada ya watoto hao kwenda kuogelea wakiwa pamoja na mama yao katika bwawa la hoteli hiyo.
“Tunaomba mamlaka husika ziwachukulie hatua wamiliki wa hoteli hiyo ili kubaini kama kulikuwa na udhibiti wa kutosha kwa watoto waliokuwa wakiogelea,” alisema Meliyo.
Aliongeza kuwa mazishi ya watoto hao yanatarajiwa kufanyika Jumamosi nyumbani kwa marehemu kijijini Kimnyaki, huku maandalizi yakiendelea katikati ya huzuni kubwa.
Wakati huo huo, taarifa kutoka Jeshi la Polisi jijini Arusha zinaeleza kuwa watu wanne wanashikiliwa, akiwemo mmiliki wa hoteli hiyo, kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo, wakati uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo halisi na iwapo kulikuwa na uzembe wa kibinadamu au ukiukwaji wa taratibu za usalama.
— Mwisho —















0 Comments