Katambi Aagiza Kupunguzwa Urasimu Ili Kukuza Biashara na Viwanda
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, ameielekeza menejimenti ya wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake kuimarisha kwa vitendo utekelezaji wa sera na sheria, sambamba na kuboresha mifumo ya usimamizi wa biashara, ili kupunguza urasimu usio wa lazima unaokwamisha utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha menejimenti kilicholenga kufanya tathmini ya utendaji wa wizara na taasisi zake, kilichofanyika Januari 8, 2026 jijini Arusha, Katambi alisema maboresho hayo ni nguzo muhimu katika kujenga mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji.
Alisisitiza kuwa sekta binafsi si mshindani wa serikali, bali ni mshirika wa kimkakati katika kutatua changamoto na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia viwanda na biashara. Kwa mujibu wake, mafanikio ya ajenda ya uchumi wa viwanda yanategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi.
Naibu Waziri huyo alieleza kuwa mifumo ya udhibiti na usimamizi wa biashara inapaswa kuwa rahisi, wazi na inayotabirika, huku ikiruhusu majadiliano ya mara kwa mara na wadau wa sekta binafsi. Alisema hatua hiyo itahakikisha sera zinakuwa shirikishi na zenye majibu ya moja kwa moja kwa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.
Aidha, Katambi alibainisha kuwa utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara na wawekezaji lazima uzingatie misingi ya uwazi na ushirikishwaji, ikiwemo kutoa fursa kwa sekta binafsi kupendekeza maboresho ya mifumo na mabadiliko ya sheria ili kuondoa vikwazo vinavyolalamikiwa mara kwa mara katika mazingira ya biashara.
Aliongeza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya wizara, taasisi na sekta binafsi ni sharti la msingi la kufanikisha maendeleo ya uchumi wa taifa, akisisitiza kuwa serikali inapaswa kuona sekta binafsi kama mshiriki muhimu katika safari ya maendeleo, si mpinzani.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, alisema kikao kazi hicho ni muhimu katika kuhakikisha malengo ya kimkakati ya wizara yanafikiwa. Alitaja malengo hayo kuwa ni pamoja na kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya viwanda, kuongeza ajira, kuboresha upatikanaji wa mitaji, pamoja na kuhamasisha ubunifu na uvumbuzi ili kuimarisha ushindani wa viwanda vya ndani.
Mwisho.


0 Comments