TWARIQA ARUSHA YAMSHUKURU MBUNGE MAKONDA KWA MSAADA ULIOGUSA MAMIA YA WAOMBOLEZAJI WA KIFO CHA SHEIKH ROCKET, WAMSHUKURU SAMIA KWA KUMPA U-WAZIRI


TWARIQA YAMPA MAKONDA HESHIMA MAALUM KWA KUWAGUSA WAOMBOLEZAJI WA SHEIKH ROCKET

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA

TAASISI ya Dini ya Kiislamu ya Twariqa Mkoani Arusha imeeleza shukrani zake za dhati kwa Mbunge wa Arusha Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kwa kutoa msaada wa chakula uliowawezesha waumini na waombolezaji kushiriki kikamilifu shughuli za kumuombea dua kiongozi wao marehemu, Sheikh Daruwesh Ali bin Mussa maarufu Sheikh Rocket.

Akizungumza leo januari 21,2026 katika Zawiya Kuu ya Twariqa Arusha, Naibu Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Haruna Husein, alisema Makonda ametoa kilo 100 za mchele kupitia ofisi ya Mbunge Arusha Mjini, mchango ambao umeanza kutumika rasmi katika chakula cha waumini waliokusanyika kwa ajili ya dua, Swala ya Janaza ya ghaibu na maombolezo ya siku kadhaa.

 
Marehemu sheikh Rocket

“Kwa mapenzi na rehema za Mwenyezi Mungu tumepokea mchango huu muhimu kwa wakati muafaka. Umewekwa chini ya uangalizi wa viongozi wetu wakuu akiwemo Halifa Kiongozi na Kamati ya Fedha ya Taasisi. Ni msaada uliogusa mahitaji halisi ya waumini,” alisema Sheikh Haruna.

Alieleza kuwa kifo cha Sheikh Rocket kilitokea tarehe 19 Januari 2026, na mazishi kufanyika mkoani Mtwara, hali iliyosababisha waumini wengi walioko Kanda ya Kaskazini kushindwa kuhudhuria kutokana na umbali, hivyo Twariqa ikaandaa dua na maombolezo maalum jijini Arusha.

Sheikh Haruna alisema msaada wa Makonda unaakisi mshikamano wa kijamii na kidini, na unaonesha namna viongozi wa kisiasa wanavyoweza kushiriki kwa vitendo katika kugusa maisha ya waumini, hususan katika nyakati za misiba.

“Twariqa ina kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Paul Makonda kwa kuendelea kuunga mkono shughuli za kijamii na kidini. Huu ni mfano wa uongozi unaogusa watu,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Sheikh Haruna alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kumuamini Makonda kwa kumpa dhamana ya kuiongoza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, akisema taasisi hiyo ina imani kuwa ataitumikia wizara hiyo kwa uadilifu, weledi na uzalendo.

Kwa niaba ya viongozi na waumini wa Twariqa, alisema wanaendelea kumuombea Makonda dua ili Mwenyezi Mungu amjaalie afya njema, hekima na mafanikio katika majukumu yake ya kibunge na kitaifa, huku akiwasihi waumini kuendeleza mshikamano, subira na amani.

Kwa upande wake, Katibu wa Ofisi ya Mbunge Arusha Mjini, Antony Maswi, alisema msaada huo umetoka ofisi ya mbunge kwa lengo la kushiriki maombolezo na kuwafariji waumini wa Twariqa katika kipindi hiki cha msiba huo mzito.

Marehemu sheikh Rocket

WASIFU NA HISTORIA FUPI YA MAREHEMU SHEIKH DARUWESH ALI BIN MUSSA (SHEIKH ROCKET)

Marehemu Sheikh Daruwesh Ali bin Mussa, maarufu kama Sheikh Rocket au “Kuswali Nnaleke”, alizaliwa mwaka 1928 (au 1930 kwa baadhi ya riwaya) katika kijiji cha Momburu, Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara.

Awali alilelewa katika mazingira ya Kikristo kabla ya kuikubali dini ya Kiislamu. Aliwahi kujiunga na Jeshi la Polisi la Tanganyika, akihudumu katika mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha na Lindi, na kufikia cheo cha Mkuu wa Kituo cha Polisi.

Safari yake ya kiroho ilianza baada ya kukutana na masheikh wa tasawwuf, akiwemo Sheikh Daruwesh Mti Mkavu na Al-Habib Sheikh Muhammad bin Nassor (RahimahuLlah). Baada ya kusilimu rasmi alipata ijaza na ruhusa ya kuhubiri, na akaanza kujulikana kwa wito wake maarufu:

“KUSWALI NNALEKE – USIACHE KUSWALI.”


Mwaka 1966, aliacha kabisa kazi ya uaskari na kujitosa kikamilifu katika da‘wah na tasawwuf. Alisafiri hadi Lamu, Kenya, ambako alipata ijaza ya Twariqatul Alawiyya, na aliripotiwa kuhiji zaidi ya mara 50 mfululizo.

Sheikh Rocket alijenga na kusimamia ujenzi wa misikiti kadhaa, ikiwemo Msikiti Mkuu wa Ijumaa Ndanda (Mtwara), na alifanya da‘wah ndani na nje ya Tanzania, akiwafikishia ujumbe wa Uislamu maelfu ya watu.

Marehemu aliacha wake sita, watoto 40 na wajukuu 75. Alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, na atakumbukwa kama askari aliyebadilika kuwa daruwesh na da‘i aliyedumisha wito wa imani kwa maneno yake ya urithi:

“KUSWALI NNALEKE.”








Post a Comment

0 Comments