Na Joseph Ngilisho – ARUMERU.
Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Nicholas Francis, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Malalua–Nduruma–Bwawani unaendelea vizuri na umefikia asilimia 73.18 ya utekelezaji, huku sehemu ya kilomita 0.65 ikijengwa kwa kiwango cha lami.
Alitoa taarifa hiyo jana wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (Elimu), Reuben Kwagilwa, Januari 17, 2026, katika Halmashauri ya Arusha(Arusha DC) wilayani Arumeru.
Akizungumza katika ziara hiyo ya ukaguzi, Mhandisi Francis alisema mradi huo ni sehemu ya ujenzi wa jumla ya kilomita 27.949 za barabara ya Malalua–Nduruma–Bwawani, unaotekelezwa kupitia Mfuko wa Barabara (Road Fund Development).Alisema ujenzi wa kipande cha lami cha kilomita 0.65 unatekelezwa na kampuni ya M/S Afritrust Company Ltd kwa gharama ya shilingi milioni 700, fedha za Serikali.
Alifafanua kuwa utekelezaji wa mradi ulianza rasmi Septemba 13, 2024 na unatarajiwa kukamilika Aprili 16, 2026.
Hadi sasa, kazi zilizotekelezwa ni pamoja na uundaji wa matabaka ya barabara, ujenzi wa makalavati makuu matatu, uwekaji wa lami mita 650 pamoja na ujenzi wa makalavati madogo matatu ya kupitisha miundombinu mbalimbali, kazi ambazo zote zimekamilika kwa kiwango kinachoridhisha.
Kuhusu masuala ya kifedha, Meneja huyo wa TARURA Mkoa wa Arusha alisema mkandarasi hadi sasa amelipwa kiasi cha shilingi 157,387,490, sawa na asilimia 22.48 ya gharama zote za mradi.
Alibainisha kuwa TARURA inaendelea kufuatilia malipo kwa mujibu wa hatua za utekelezaji ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Hata hivyo, alieleza kuwa mradi umekumbana na changamoto kadhaa, ikiwemo kuchelewa kuhamishwa kwa miundombinu ya moto inayotumika kwenye shughuli za kilimo pamoja na uhaba wa lami nchini uliosababisha kupanda kwa bei ya malighafi hiyo muhimu ya ujenzi wa barabara.
Akizungumzia utatuzi wa changamoto hizo, Mhandisi Francis alisema TARURA kwa kushirikiana na wadau wa mashamba waliweza kuhamisha miundombinu iliyokuwa inakwaza utekelezaji wa mradi, hatua iliyowezesha kazi kuendelea.
Aidha, alisema hali ya upatikanaji wa lami nchini imeanza kurejea katika hali ya kawaida, jambo linalotarajiwa kuongeza kasi ya kukamilisha mradi kwa wakati uliopangwa.
Katika hitimisho lake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo ambao utawanufaisha wananchi wa Wilaya ya Arusha kiuchumi na kijamii.
Pia alimshukuru Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa kutembelea, kukagua na kutoa maelekezo yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa miradi ya barabara katika mkoa huo.
Ends .


0 Comments