MBUNGE LUKUMAY AIBUA CHANGAMOTO ZA BARABARA, ELIMU NA MAJI ARUMERU MAGHARIBI,NAIBU WAZIRI KWAGILWA ATOA MAAGIZO MAZITO KWA TARURA KUZINGATIA KAULI YA MBUNGE

MBUNGE LUKUMAY AIBUA CHANGAMOTO ZA BARABARA, ELIMU NA MAJI ARUMERU MAGHARIBI

Na Joseph Ngilisho – ARUMERU


MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameiomba Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (Elimu) kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto za miundombinu ya barabara, elimu na maji safi na salama zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.


Dkt. Lukumay aliyasema leo januari 17,2026 wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (Elimu), Reuben Kwagilwa, alipotembelea jimbo hilo kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Akizungumzia barabara, alisema wananchi wa Nduruma wanakabiliwa na changamoto ya barabara ya Malalua–Nduruma ambayo hadi sasa imejengwa kwa kiwango cha lami kwa kilometa 0.6 pekee.


 Aliomba iongezwe angalau kilometa tano hadi Bwawani ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na upatikanaji wa huduma za kijamii, akibainisha kuwa wakati wa mvua barabara na madaraja huwa katika hali mbaya.

Hata hivyo, aliipongeza Serikali kwa kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 16.2 katika miradi ya barabara jimboni humo, ikiwemo Otulmenti (km 1) inayohudumia Hospitali ya Wilaya, Sekei–Oligilai (km 1) na Sanawari–Oldonyo–Sapuko (km 3). Pia aliomba ujenzi wa barabara ya kilometa moja kuelekea Shule ya Sekondari Ilboru kutokana na umuhimu na historia ya shule hiyo.


Aidha, alitaja changamoto ya barabara ya Mbauda–Oljoro–Losinyai ambayo imekuwa ikikwama kwa muda mrefu, hali inayowanyima wananchi wa Oljoro, Losinyai na Aparalwe fursa ya kunufaika na mazao yao. 


Katika eneo la madaraja, aliomba ujenzi na ukarabati wa madaraja ya Mbuyuni, Mirongoinne na Timbolo Forest ili kuwezesha shughuli za kiuchumi na usafiri salama.


Katika sekta ya elimu, aliipongeza Serikali kwa kuboresha Shule ya Sekondari Kiutu, lakini akaeleza bado kuna changamoto katika shule kadhaa, ikiwemo Shule ya Sekondari Losinoni ambako wanafunzi hutembea umbali mrefu huku wakikabiliwa na hatari ya wanyamapori.


 Aliomba Shule ya Sekondari Olmotonyi ijengewe madarasa manne na bweni moja ili iweze kupandishwa hadhi kuwa shule ya kidato cha tano na sita, pamoja na kukamilishwa kwa maboma manane ya madarasa katika Shule ya Sekondari Losikito na shule nyingine mbili.


Kwa upande wa shule za msingi, alisema zaidi ya shilingi bilioni 1.7 zimewekezwa katika ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu, lakini changamoto ya makazi ya walimu bado ni kubwa, akitolea mfano Shule ya Msingi Imayani ambako walimu husafiri zaidi ya kilometa sita.


Kuhusu maji, Dkt. Lukumay alisema licha ya kuwepo kwa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 520, kata kadhaa zikiwemo Arumeru, Sambasha, Kimnyaki, Olmotonyi, Kiranyi, Tarakwa, Olorien na Kiutu bado hazijanufaika ipasavyo. Aliomba Serikali ihakikishe wananchi wananufaika na mradi huo, hasa kutokana na changamoto ya maji yenye madini ya fluoride yanayoathiri afya.


Mwisho, aliishukuru Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa wananchi wa Arumeru Magharibi wana matumaini makubwa kuwa changamoto zao zitaendelea kupatiwa ufumbuzi.


Naibu Waziri wa TAMISEMI (Elimu),  Reuben Kwagilwa, amesisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji, na usimamizi makini katika maandalizi ya bajeti za elimu na maendeleo ya serikali za mitaa. 


Alibainisha kuwa bajeti ya sekta husika imeongezeka kutoka shilingi bilioni 275 hadi takribani shilingi trilioni 1.1, jambo linalohitaji ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa viongozi wa mikoa na wilaya ili kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa ufanisi na zinawafikia wananchi ipasavyo.


Alieleza kuwa taarifa zote kutoka kwa Wakuu wa Wilaya, Wabunge, na vyombo vinavyohusiana na utekelezaji wa bajeti lazima ziwasilishwe mapema. Hii itatoa fursa ya ushauriano wa pamoja, kupanga vipaumbele vya msingi, na kuzingatia changamoto zote zinazoweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya elimu na miundombinu ya jamii.


Akizungumza kuhusu Tarura, Naibu Waziri aliweka msisitizo mkubwa juu ya miundo miwili ya huduma na miundombinu, akibainisha kuwa miundo hii ni msingi wa utekelezaji wa miradi ya kimsingi ya elimu na maendeleo ya mitaa. 


Alisisitiza kuwa kuzingatia miundo yote kunahakikisha bajeti inatekelezwa kwa ufanisi, miradi inakamilika kwa wakati, na huduma zinazofikia wananchi zinaboreshwa.


Kwagilwa aliwahakikishia  Wabunge kuwa mradi mkubwa wa shilingi bilioni 520 unaendelea kufuatiliwa kwa karibu, huku akisisitiza kuwa hatua zote muhimu zimezingatiwa. 


Uangalizi maalumu wa miundo mbinu unalenga kuhakikisha miradi ya Tarura inakamilika kikamilifu, inaboresha maisha ya wananchi, na inalingana na malengo ya kitaifa ya elimu na maendeleo ya jamii.




Ends...


Post a Comment

0 Comments