NGOBEI ACHAGULIWA MWENYEKITI MPYA ALAT ARUSHA, HALMASHAURI ZATAKIWA KULIPA MADENI YA SH MILIONI 103.5
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Thomas Ngobei, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Arusha, katika uchaguzi uliofanyika kwenye kikao maalum cha jumuiya hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Jiji la Arusha.
Katika uchaguzi huo, nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilichukuliwa na Lucas Kaaya ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru huku nafasi ya Katibu wa ALAT Mkoa wa Arusha ikichukuliwa na Juma Hokololo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa, Mwenyekiti mpya wa ALAT Mkoa wa Arusha, Thomas Ngobei, alisisitiza umuhimu wa jumuiya hiyo kama jukwaa la pamoja la kusimamia na kusukuma mbele maendeleo ya halmashauri, kuimarisha mshikamano baina ya serikali za mitaa na kusimamia maslahi yao kwa ufanisi.
Ngobei alizitaka halmashauri zote zinazounda ALAT Mkoa wa Arusha kuonesha uwajibikaji wa kifedha kwa kulipa madeni ya michango yanayodaiwa na jumuiya hiyo, akieleza kuwa hali ya kuchelewesha au kutolipa michango imekuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa majukumu ya ALAT.
Kwa mujibu wa taarifa ya ALAT Mkoa wa Arusha, jumuiya hiyo inaendelea kukabiliwa na changamoto ya ukusanyaji wa michango kutoka baadhi ya halmashauri na taasisi zake, hali inayodhoofisha shughuli zake za msingi ikiwemo uratibu wa shughuli za serikali za mitaa, utetezi wa maslahi yao na uimarishaji wa utawala bora katika ngazi za chini.
Katika mchanganuo wa madeni, Halmashauri ya Jiji la Arusha imepongezwa kwa kuonesha nidhamu nzuri ya kifedha katika mwaka wa fedha 2024/25 ambapo haina deni lolote, ingawa kwa mwaka wa fedha 2025/26 bado haijalipa mchango wa shilingi milioni 8 unaostahili.
Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC) inadaiwa shilingi milioni 8 kwa mwaka wa fedha 2024/25 na shilingi milioni 6 kwa mwaka 2025/26, hivyo kufanya jumla ya deni lake kufikia shilingi milioni 14. Halmashauri ya Meru nayo inadaiwa shilingi milioni 8.5 kwa mwaka 2024/25 na shilingi milioni 6 kwa mwaka 2025/26, jumla ya shilingi milioni 14.
Kwa upande wa Halmashauri ya Ngorongoro, ilitakiwa kulipa shilingi milioni 18.5 kwa mwaka wa fedha 2024/25 na shilingi milioni 6 kwa mwaka 2025/26, lakini hadi sasa imelipa shilingi milioni 2 pekee, na kubaki na deni la jumla ya shilingi milioni 22.5.
Halmashauri ya Monduli imeongoza kwa kuwa na deni kubwa zaidi, ikidaiwa shilingi milioni 18 kwa mwaka wa fedha 2024/25 na shilingi milioni 6 kwa mwaka 2025/26 bila kulipa kiasi chochote, hivyo jumla ya deni lake kufikia shilingi milioni 24.
Halmashauri ya Karatu inadaiwa shilingi milioni 4 kwa mwaka 2024/25 na shilingi milioni 6 kwa mwaka 2025/26, jumla ya shilingi milioni 10, huku Halmashauri ya Longido ikidaiwa shilingi milioni 9.5 kwa mwaka 2024/25 na shilingi milioni 4 kwa mwaka 2025/26, jumla ya shilingi milioni 10.5.
Kwa ujumla, ALAT Mkoa wa Arusha imesema kuwa jumla ya deni la michango kwa mwaka wa fedha 2024/25 linafikia shilingi milioni 63.5 na kwa mwaka wa fedha 2025/26 ni shilingi milioni 42, huku kiasi kilicholipwa hadi sasa kikiwa shilingi milioni 2 pekee. Hivyo, jumla ya michango inayodaiwa kufikia shilingi milioni 103.5.
Wakati huo huo, Makamu Mwenyekiti mpya wa ALAT, Lucas Kaaya, alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa fursa ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo ya uongozi, sambamba na kuwashukuru wajumbe wa jumuiya hiyo kwa kumuamini na kumpigia kura nyingi.
Kaaya alisema dhamana aliyopewa ni kubwa na inahitaji uadilifu, uwajibikaji na mshikamano wa hali ya juu, huku akiahidi kusimamia kikamilifu maslahi ya halmashauri zote kwa kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinafuatwa, na maamuzi yanazingatia hali halisi na changamoto zilizopo.
Ameeleza kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kutetea haki na maslahi ya madiwani, hususan katika eneo la posho na mazingira ya kazi, akisisitiza kuwa madiwani wanapaswa kuthaminiwa kwa kuzingatia uzito wa majukumu wanayoyatekeleza kwa niaba ya wananchi.
Aidha, Kaaya alisema uongozi wake utaimarisha ushirikiano kati ya mwenyekiti, kamati za halmashauri na wadau mbalimbali, kwa lengo la kuimarisha kamati za kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
ALAT Mkoa wa Arusha imezitaka halmashauri zote zenye madeni kuchukua hatua za haraka kulipa michango yao, ili kuiwezesha jumuiya hiyo kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kuendelea kutetea maslahi ya serikali za mitaa kwa maendeleo ya wananchi.
Ends..













0 Comments