Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limefanikiwa kumkamata mtu mmoja raia wa Kenya kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa kuvunja na kuingia katika tawi la Benki ya Azania lililopo mji wa Namanga, wilayani Longido, mkoani Arusha.
Akitoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo, amesema mtuhumiwa huyo ametambuliwa kwa jina la Denis Ogesa, mwenye umri wa miaka 28, mkazi wa Nairobi nchini Kenya.
SACP Masejo amesema tukio hilo lilitokea Januari 14, 2026 majira ya saa 6:40 usiku, ambapo mtuhumiwa alifanikiwa kuvunja na kuingia katika jengo la benki hiyo kwa nia ya kufanya wizi, kinyume cha sheria za nchi.
Ameeleza kuwa wakati mtuhumiwa huyo akiendelea kutekeleza tukio hilo la kihalifu, askari wa Jeshi la Polisi walifanikiwa kumkamata akiwa ndani ya benki hiyo, hatua iliyozuia hasara kubwa zaidi inayoweza kujitokeza.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Polisi, mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa tayari na fedha taslimu zilizodaiwa kupatikana ndani ya benki hiyo, zikiwemo fedha za Kitanzania kiasi cha Shilingi 91,280,000/= pamoja na fedha za Kenya zenye thamani ya Shilingi 288,700/= (Kshs).
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limeeleza kuwa linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini iwapo mtuhumiwa huyo alikuwa na washirika wengine katika tukio hilo, hususan kutokana na mazingira ya tukio na kiasi cha fedha kilichokutwa nacho.
SACP Masejo amesisitiza kuwa baada ya uchunguzi kukamilika, mtuhumiwa pamoja na mtu au watu wengine watakaobainika kuhusika watafikishwa mahakamani ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Kamanda huyo ametoa wito kwa taasisi za fedha na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za kiintelijensia zitakazosaidia kuzuia na kudhibiti vitendo vya uhalifu, hasa katika maeneo ya mipakani ambayo yana mwingiliano mkubwa wa watu kutoka mataifa jirani.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limewahakikishia wananchi kuwa linaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha usalama wa mali na raia, na halitasita kuwachukulia hatua kali wote wanaojihusisha na vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa nchi.
Ends..

0 Comments