MOTO WATEKETEZA MADUKA NA KARAKANA MOSHONO, HASARA YAFIKIA BILIONI 1
Na Joseph Ngilisho – Arusha
MOTO mkubwa umezuka usiku wa kuamkia leo Januari 26, 2026 katika eneo la Moshono, jijini Arusha, na kuteketeza maduka kadhaa, karakana nane za mbao pamoja na timber nyingi, na kusababisha hasara kubwa ya mali inayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 1.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, moto ulianza majira ya saa tisa usiku na kuenea kwa kasi kubwa kutokana na uwepo wa vifaa vinavyoshika moto kwa urahisi, hususan mbao, timber na rangi zilizokuwa zikitumika kwenye karakana hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari, mmoja wa mashuhuda Godfrey Mollel, mfanyabiashara wa eneo hilo, amesema walishitushwa na mlipuko wa ghafla wa moto uliokuwa tayari umeenea kabla hawajapata msaada.
“Tuliona moshi mzito ukipanda juu kisha moto ukaenea kwa kasi sana, ndani ya dakika chache karakana zote zilikuwa zinawaka. Tulijaribu kuokoa baadhi ya vifaa lakini haikuwezekana,” amesema Mollel.
Mashuhuda wengine wamesema kilio na makelele ya wananchi yalitanda eneo hilo huku baadhi ya wafanyabiashara wakishuhudia mali zao zikiteketea bila msaada wa haraka kutokana na ukubwa wa moto.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Arusha lilifika eneo la tukio na kuanza jitihada za kuzima moto huo, ambapo baada ya mapambano ya muda mrefu, moto ulifanikiwa kudhibitiwa asubuhi ya leo.
Kamanda wa jeshi la Zimamoto na uokozi Mkoa wa Arusha ,Oswald Mwanjele amesema kuwa hadi sasa hakuna taarifa za majeruhi wala vifo, huku uchunguzi wa kina ukiendelea kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.
“Taarifa za awali zinaonyesha kuwa chanzo cha moto huenda kilitokana na hitilafu ya umeme, hata hivyo uchunguzi bado unaendelea ili kuthibitisha rasmi,” amesema.
Wananchi wa Moshono wameitaka serikali na mamlaka husika kuongeza ukaguzi wa mifumo ya umeme katika maeneo ya biashara, hususan yale yanayotumia vifaa vinavyoshika moto kwa urahisi, ili kuzuia majanga kama hayo kujirudia.
Moto huo umeacha majonzi kwa wafanyabiashara waliopoteza mitaji na vyanzo vyao vya kipato, huku juhudi za tathmini ya kina ya hasara zikitarajiwa kuendelea katika siku chache zijazo.





0 Comments