DKT LUKUMAY AIPIGIA DEBE BIMA YA AFYA KWA WOTE ASISITIZA NI MAGEUZI MAKUBWA SEKTA YA AFYA NCHINI,ATAKA SERIKALI KUHARAKISHA MABORESHO

LUKUMAY AIPIGIA DEBE AFYA KWA WOTE: BIMA YA AFYA SI KAULIMBIU, NI HAKI YA MSINGI YA MWANANCHI

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA


MWENYEKITI  wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya, Dkt. Johannes Lukumay, ametoa wito  kwa Serikali kuharakisha maboresho ya sekta ya afya nchini, akisisitiza kuwa Bima ya Afya kwa Wote si mpango wa takwimu wala sera ya kisiasa, bali ni haki ya msingi ya kila Mtanzania kupata huduma bora za afya bila kujali hali yake ya kiuchumi.

Dkt. Lukumay ameyasema hayo leo januari 26,2026  jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa mawasiliano kati ya wananchi na Waziri wa Afya, hafla iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru na kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa.


Akizungumza kwa msisitizo, Dkt. Lukumay ambaye pia ni mbunge wa Arumeru Magharibi Mkoani hapa,amesema kuwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unapaswa kuonekana kwa vitendo, si kwa maneno, kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa wakati, kwa ubora na bila vikwazo, hususan makundi yenye uhitaji mkubwa yakiwemo kaya maskini, watoto chini ya miaka mitano, akina mama wajawazito, wazee na wananchi wanaoishi katika mazingira magumu.

“Akili ya Mtanzania haiwezi kupuuzia suala hili nyeti la Bima ya Afya kwa Wote. Maana yake halisi ni kuhakikisha kila mwananchi, bila kujali kipato chake, anapata huduma bora za afya bila kubaguliwa wala kunyanyapaliwa,” amesema Dkt. Lukumay.

Akielekeza ujumbe wake moja kwa moja kwa Waziri wa Afya, Dkt. Lukumay amesisitiza kuwa afya njema ya wananchi ndiyo injini ya uzalishaji, ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi wa taifa, akionya kuwa bila wananchi wenye afya, ndoto ya maendeleo haiwezi kufikiwa.

“Mheshimiwa Waziri, jukumu lako ni kubwa. Afya ndiyo nguzo ya maendeleo ya taifa. Bila wananchi wenye afya njema, hatuwezi kufikia malengo yetu ya kiuchumi na kijamii,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa dira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kuona kila Mtanzania, popote alipo, anapata huduma bora za afya, na kwamba hiyo ndiyo Tanzania inayotakiwa—ambayo wagonjwa hawateseki kwa kukosa matibabu na maskini hawabaguliwi .

Katika hotuba yake, Dkt. Lukumay hakusita kuibua changamoto zinazoendelea kuikabili sekta ya afya, zikiwemo upungufu wa vifaa tiba muhimu kama mashine za X-ray, ucheleweshaji wa utoaji wa fedha licha ya bajeti kupitishwa na miradi ya afya pamoja na viwanda vya dawa kutokutumika ipasavyo.

Ametolea mfano hoja zinazohusu matumizi ya bajeti ya shilingi bilioni 6.6, ikiwemo ucheleweshaji wa utoaji wa shilingi bilioni 1.5 kwa huduma za watoto wengi, hali inayosababisha huduma bora kushindikana kuwafikia wananchi walengwa.

“Haina maana kununua mashine ghali halafu zinafungwa au hazifanyi kazi. Wananchi wanahitaji huduma, si majengo wala vifaa vilivyofungwa,” amesisitiza.


Kwa mujibu wa Dkt. Lukumay, uwekezaji katika sekta ya afya una faida pana zaidi ya utoaji wa tiba, kwani unachochea ajira, kuimarisha uchumi na kupunguza mateso ya wananchi.

“Wageni na wawekezaji wanaweza kuja na kuondoka, lakini maendeleo ya kweli huanza na wananchi wenye afya njema,” amesema.

Akihitimisha, Dkt. Lukumay amemtaka Waziri wa Afya kuhakikisha vituo vya afya vinawekewa vifaa muhimu, mashine zinafanya kazi ipasavyo na wananchi wanapata huduma kwa wakati bila usumbufu usio wa lazima.

Pia amempongeza Waziri Mchengerwa kwa kuanzisha mfumo wa kidigitali wa mawasiliano kati ya wananchi na Wizara ya Afya, akisema kuwa mfumo huo utaimarisha uwazi, uwajibikaji na kushirikisha wananchi moja kwa moja katika kuboresha huduma za afya.

“Tukiunganisha nguvu za serikali, chama na wananchi, tunaweza kubadilisha kabisa maisha ya Watanzania,” amehitimisha Dkt. Lukumay.

Ends...


Post a Comment

0 Comments