MCHENGERWA AIPONGEZA SPANISH TILES KWA UJENZI WA JENGO LA SARATANI ARUSHA, AAGIZA HUDUMA KUANZA NDANI YA WIKI MBILI
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameipongeza taasisi ya Spanish Tiles kwa mchango wake mkubwa wa kufanikisha ujenzi wa Jengo la Huduma za Saratani litakalohudumia Mkoa wa Arusha pamoja na mikoa ya jirani, akieleza kuwa uwekezaji huo ni kielelezo cha ushirikiano chanya kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya nchini.
Waziri Mchengerwa alitoa pongezi hizo leo Januari 26, 2026, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la jengo hilo linalojengwa kwa ufadhili wa Spanish Tiles katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha – Mount Meru.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mchengerwa alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, kuhakikisha kuwa ndani ya wiki mbili vifaa vyote vya matibabu vinakuwa vimefikishwa hospitalini hapo ili wananchi waanze kunufaika mara moja na huduma za matibabu ya saratani.
“Hatuna sababu ya kuchelewesha huduma hizi. Vifaa vikishafika, Watanzania waanze kutibiwa hapa hapa Arusha bila kusafiri umbali mrefu,” alisisitiza Waziri Mchengerwa.
Aidha, Waziri huyo aliishukuru Spanish Tiles chini ya uongozi wa Mkurugenzi wake, Bw. Bobby Chadha, kwa kujitolea kugharamia ujenzi wa jengo hilo, akibainisha kuwa mchango huo utaokoa maisha ya wananchi wengi na kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za matibabu.
Mchengerwa pia alitoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji wengine kuiga mfano huo kwa kuwekeza katika sekta ya afya, akieleza kuwa ushiriki wa sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kufanikisha azma ya Serikali ya kuboresha huduma za afya kwa wote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Spanish Tiles, Bobby Chadha, akitoa salamu za kampuni hiyo, aliishukuru Serikali kwa mazingira mazuri ya ushirikiano na wadau wa maendeleo, akieleza kuwa kampuni hiyo imeguswa na wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.
Bw. Chadha alisema uamuzi wa kampuni hiyo kuchangia ujenzi wa jengo la saratani Arusha umetokana na umuhimu wa mkoa huo, hususan kutokana na uwepo wa watalii wengi pamoja na ongezeko la mahitaji ya huduma za afya za kibingwa.
“Tumeona ni wajibu wetu kama wadau wa maendeleo kushirikiana na Serikali kusogeza huduma hizi muhimu karibu na wananchi,” alisema Bw. Chadha.
Katika hatua nyingine, Bw. Chadha aliridhia ombi la Waziri Mchengerwa, ambapo Waziri huyo alimweleza kuwa Serikali iko tayari kumuonesha maeneo mengine yenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya ili kampuni hiyo iweze kuwekeza zaidi na kusogeza huduma hizo kwa wananchi wengi zaidi.
Kukamilika kwa jengo hilo la huduma za saratani kunatarajiwa kuokoa muda na gharama kubwa za matibabu kwa wananchi, ambao hapo awali walilazimika kusafiri hadi Hospitali ya Ocean Road Dar es Salaam au nje ya nchi kupata huduma hizo. Sasa, huduma za kibingwa za saratani zitapatikana ndani ya Mkoa wa Arusha, hatua itakayopunguza mzigo wa kiuchumi na kuongeza ufanisi wa matibabu.








0 Comments