MBUNGE KADOGOO ALIA NA MATESO YA MAJI NA MALISHO , AOMBA SERIKALI KUOKOA WAFUGAJI MONDULI


MBUNGE KADOGOO ALIA NA MATESO YA MAJI, AOMBA SERIKALI KUOKOA WAFUGAJI MONDULI

Na Joseph Ngilisho – MONDULI

MBUNGE wa Jimbo la Monduli, Joseph Isack Maarufu Kadogoi, amelia kwa uchungu mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makala, akieleza mateso makubwa yanayowakumba wananchi wa Monduli kutokana na ukosefu wa maji na uhaba wa malisho, akisema hali hiyo imeendelea kuwa kilio cha muda mrefu kwa wafugaji na jamii nzima ya wilaya hiyo.

Kadogoi alitoa kauli hiyo wilayani Monduli wakati wa ziara ya kikazi ya Mkuu wa Mkoa Makala, aliyefika kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi, ambapo suala la maji na malisho lilijitokeza kama ajenda kuu ya mbunge huyo kikao hicho.




Akizungumza kwa msisitizo, Mbunge huyo alisema maji ndiyo agenda yake kubwa kwa kipindi chake cha uongozi, akibainisha kuwa kwa miaka mingi wananchi wa Monduli wamekuwa wakiahidiwa miradi ya maji bila mafanikio ya kudumu.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, agenda yangu kwa miaka yangu mitano ya uongozi ni moja tu—maji, maji na maji. Wananchi wa Monduli wamechoka mateso. Bila maji hakuna maisha, hakuna mifugo, hakuna maendeleo,” alisema Kadogoi.

Kadogoi alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumteua CPA Makala kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, akisema uteuzi huo umeleta matumaini mapya kwa wananchi wa mkoa huo, hususan wilaya ya Monduli.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuona wananchi wa Arusha na kutuletea uongozi imara. Tunakupongeza Mheshimiwa Makala, na tuna imani utakuwa daraja la kutufikisha kwenye suluhisho la changamoto zetu,” alisema.

Akizungumzia mradi wa maji wa Munduli, Kadogoi alisema tayari amekutana na wakandarasi wanaotekeleza mradi huo pamoja na uongozi wa halmashauri, na kwamba wamewasilisha ratiba na mpango wa utekelezaji unaotia matumaini, licha ya kuwepo kwa changamoto ndogondogo.

“Wengi wameanza mradi huu kabla yetu, lakini haujakamilika. Natamani katika kipindi chetu tuandike historia kwa kuukamilisha. Huu ni mradi wa kizazi cha sasa na kijacho,” alisisitiza.

Mbunge huyo pia aliipongeza Serikali kwa uwazi kuhusu mchakato wa kusainiwa kwa mikataba ya utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa tayari ameshuhudia vielelezo vya uzalishaji wa mabomba, na ameomba hata kupata fursa ya kwenda kushuhudia uzalishaji huo kwa macho yake mwenyewe ili kuhakikisha mradi haukwami njiani.

Katika hatua nyingine, Kadogoi aligusia kwa uzito suala la malisho kwa wafugaji, akisema kuwa hilo ni tatizo nyeti kwa jamii ya Monduli ambayo maisha yake yanategemea ufugaji.

“Kama wafugaji, tunachohitaji zaidi ni malisho. Hili nilimwomba hata Mheshimiwa Rais, naye aliahidi kulisimamia. Tunaomba ofisi ya Mkuu wa Mkoa itusaidie kulifuatilia kwa karibu,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makala, aliahidi kushirikiana na viongozi wote wa wilaya na wabunge kuhakikisha changamoto za maji na malisho zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuboresha maisha ya wananchi, hususan waishio maeneo ya pembezoni.

Ziara hiyo imeacha matumaini mapya kwa wananchi wa Monduli, wakiamini kuwa kilio chao cha muda mrefu kuhusu maji na malisho sasa kimepata masikio ya viongozi wakuu wa Serikali.

Ends..

Post a Comment

0 Comments