DC MKUDE AONGOZA ZOEZI LA USAFI HOSPITALI YA WILAYA, AIPA MSUKUMO KAMPENI YA ‘NG’ARISHA JIJI LA ARUSHA’
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ameongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Arusha katika zoezi maalum la usafi wa mazingira lililofanyika leo Januari 03, 2026 katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Kata ya Engutot,ikiwa ni sehemu ya mkakati endelevu wa kung’arisha jiji hilo na kuboresha afya ya wananchi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkude aliyekuwa ameambatana na madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, viongozi wa mitaa, kata na tarafa, alisisitiza kuwa usafi wa mazingira si tukio la siku moja bali ni ajenda endelevu inayopaswa kupewa kipaumbele cha kudumu katika maeneo yote ya jiji.
“Usafi ni jukumu la kila mmoja wetu. Ni muhimu viongozi, hususan madiwani, kuwahamasisha wananchi katika kata zao ili wajenge utamaduni wa kufanya usafi bila kusukumwa,” alisema Mkude.
Mkuu huyo wa wilaya alisema anaunga mkono kikamilifu kampeni ya ‘Ng’arisha Jiji la Arusha’ iliyoasisiwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe, na kuzinduliwa hivi karibuni katika Kata ya Sokoni One, kwa lengo la kuzifikia kata zote za jiji hilo.
Mkude alibainisha kuwa suala la usafi linapaswa kuwa ajenda ya kila siku, akisisitiza kuwa Jiji la Arusha, kama kitovu cha utalii nchini, linapaswa kuwa safi muda wote hususan ikizingatiwa kuwa linajiandaa kupokea wageni wengi katika Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Aidha, aliwataka viongozi kuendelea kuwahamasisha wananchi kuhakikisha usafi unazingatiwa katika makazi, maeneo ya biashara, masoko na maeneo ya wazi, ili kulifanya jiji kuwa safi, salama na lenye mvuto.
Akizungumzia hali ya ushindani wa usafi, Mkude alisema katika mashindano ya kitaifa ya usafi wa mazingira, Jiji la Arusha liliwahi kushika nafasi ya pili, huku akieleza kuwa mwaka 2026 analenga kuona jiji hilo likishika nafasi ya kwanza kitaifa. Aliahidi kushiriki binafsi katika zoezi la usafi katika kata zote, linalofanyika kila Jumamosi kuanzia saa moja asubuhi hadi saa nne.
Pia alieleza kuwa Serikali inasubiri kupitishwa kwa Sheria Ndogo ya Utunzaji wa Mazingira ili kuweka adhabu kali kwa wachafuzi wa mazingira, hususan wanaotupa taka ngumu ovyo, hatua itakayosaidia kudhibiti uchafuzi wa mazingira jijini.
Naye Mkuu wa kitengo Cha Uthibiti wa Taka,na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha,James Lobikoki alisema kuwa kampeni hiyo ya Usafi ni mwendelezo kuhakikisha kuwa Jiji linaendelea kung'ara,na kuhamasisha wananchi kwa kuona swalaa Usafi wa mazingira ni la kila mwananchi.
Hata hivyo ametoa rai kwa wazoa taka wa Jiji la Arusha kuendelea kufanya kazi hiyo kwa nguvu haswa katika kipindi hiki cha mvua za Vuli ili Maeneo ndani ya kataa yaendelee kuwa Safi na Salama.
Kwa upande wake, Mratibu wa zoezi la usafi Jiji la Arusha na Diwani wa Viti Maalum, Aminata Ture, kutoka Kata ya Themi, alisema kampeni hiyo inaendelea vizuri na imepokelewa kwa mwitikio chanya kutoka kwa wananchi.
“Wananchi wamehamasika kushiriki usafi katika kata zao. Tumejipanga kufika kaya mbalimbali kutoa elimu na kuhamasisha usafi wa mazingira, pamoja na kuachana na tabia ya kutupa taka ovyo,” alisema Ture.
Zoezi hilo limeonekana kuwa sehemu muhimu ya kuimarisha mshikamano kati ya viongozi na wananchi katika kulinda afya, mazingira na taswira ya Jiji la Arusha kama jiji safi na la mfano nchini.
Mwisho.



0 Comments