WATAALAM WA MIONZI WATAKIWA KUZINGATIA USALAMA WA WAGONJWA NA WATOA HUDUMA
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Watoa huduma za mionzi katika vituo mbalimbali vya afya nchini wameagizwa kuzingatia matumizi sahihi ya mionzi ili kuepuka viwango vikubwa vinavyoweza kusababisha madhara kwa wagonjwa na kwao wenyewe.
Agizo hilo limetolewa leo desemba 19,2025 jijini Arusha na Kaimu Mkuu wa Ofisi ya Kanda ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Peter Pantaleo, wakati akifunga mafunzo yaliyoshirikisha wataalam wa Radiolojia zaidi ya 90 kutoka maeneo mbalimbali nchini, yaliyoandaliwa na TAEC.
Pantaleo amesema matumizi ya kiwango kikubwa cha mionzi yana madhara makubwa zaidi ikilinganishwa na kiwango kidogo, hivyo wataalam wanapaswa kuwa makini na kufuata viwango vilivyowekwa kitaalamu ili kulinda afya za wagonjwa na watoa huduma.
Aliongeza kuwa watoa huduma za mionzi wanapaswa pia kutambua wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum zaidi, ikiwemo kuwakinga wagonjwa wanaoambatana na ndugu au wale wanaohudhuria hospitali wakati huduma za mionzi zinapotolewa.
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa wataalam wa mionzi, kwani yanawawezesha kuhakikisha usalama wao, wagonjwa wanaopata huduma pamoja na watu wengine waliopo katika mazingira ya hospitali,” alisema Pantaleo.
Kwa upande wake, mkufunzi wa mafunzo hayo, Mungubariki Nyaki, aliwataka wataalam wa Radiolojia kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa kwa kuzingatia matumizi sahihi ya mionzi sambamba na miongozo ya kitaalamu na kisheria.
Nyaki alisema TAEC itaendelea kutoa mafunzo kwa kada mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya mionzi, lengo likiwa ni kuhakikisha watoa huduma wanajikinga ipasavyo dhidi ya madhara ya mionzi, huku wagonjwa wakipata huduma salama na yenye ubora.
“Huduma za mionzi ni salama endapo zinatolewa kwa kufuata taratibu na viwango vilivyowekwa. Wagonjwa hawapaswi kuogopa kwani matumizi ya mionzi yapo chini ya udhibiti wa kitaalamu,” alisisitiza.
Wakati huohuo, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Beatrice Mallya na Hussein Shabani, wameishukuru TAEC kwa mafunzo hayo wakisema yamewasaidia kukumbushwa matumizi sahihi ya mionzi pamoja na umuhimu wa kuwa na vyumba vya kisasa na salama vya kutolea huduma hizo.
Shabani alibainisha kuwa matumizi sahihi na yenye uangalifu wa mionzi ndiyo msingi wa huduma bora kwa wagonjwa wanaofika hospitalini kupata huduma za Radiolojia.




0 Comments