SERIKALI YAIKUBALI ACFE KAMA NGUZO MUHIMU DHIDI YA UDANGANYIFU NA UBADHILIFU NCHINI

 SERIKALI YAIKUBALI ACFE KAMA NGUZO MUHIMU DHIDI YA UDANGANYIFU NA UBADHILIFU

Na Joseph Ngilisho, Arusha


Serikali imetambua mchango mkubwa wa Taasisi ya Wataalamu wa Udhibiti wa Udanganyifu Tanzania (ACFE) katika kujenga uwezo wa kitaasisi na kudhibiti vitendo vya udanganyifu na ubadhilifu nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Utumishi wa Umma na Utawala Bora leo Novemba 17,2025,Mkurugenzi wa Idara ya Maadili, Felister Shuli, alisema ACFE imekuwa chachu katika kutoa mafunzo ya kimataifa na ushauri wa kitaalamu kwa wataalamu wanaohusika na kudhibiti udanganyifu.

Alisema hayo wakati akifungua Kongamano la Mwaka la ACFE Tanzania linalofanyika jijini Arusha, likiwa na kaulimbiu “Kujenga Tanzania Imara dhidi ya Udanganyifu: Ushirikiano na Uadilifu katika Sekta Zote.”

"Taasisi hii imekuwa nguzo muhimu katika kuwajengea uwezo wataalamu wetu, hususan katika kutambua, kuchunguza na kudhibiti vitendo vya udanganyifu katika sekta za umma na binafsi," alisema Shuli.


Aliongeza kuwa juhudi za ACFE zinachangia utekelezaji wa ajenda za Serikali kuhusu utawala bora, uwajibikaji na uwazi – mambo yaliyo katika msingi wa kuhakikisha mifumo ya usimamizi wa rasilimali za umma inafanya kazi ipasavyo.

Akifafanua zaidi, Shuli alisema serikali inatekeleza maboresho makubwa ya mifumo ya usimamizi wa rasilimali hasa kupitia teknolojia ya kidijitali, ukaguzi wa kiuchambuzi na mifumo ya ufuatiliaji ndani ya taasisi za umma. Alitaja taasisi muhimu zilizomo katika juhudi hizo kuwa ni pamoja na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais Ikulu, TAKUKURU, Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Shuli alizitaka taasisi za umma na binafsi kutenga rasilimali za kutosha kwa ajili ya kuwekeza katika mafunzo na elimu ya udhibiti wa udanganyifu, kuimarisha mifumo ya fedha ya ndani, kufuata misingi ya maadili na kushirikiana kwa karibu na ACFE katika tafiti na kubadilishana taarifa za kiuchunguzi.


Kwa upande wake, Rais wa ACFE Tanzania,Ally Mabrouk Juma,alisema taasisi hiyo – iliyoanzishwa mwaka 2012 – imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Wizara ya Fedha kupitia Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali katika kujenga uwezo wa wataalamu.

“Kwa mujibu wa ripoti za kimataifa za ACFE, taasisi hupoteza takribani asilimia 5 ya mapato yake kila mwaka kutokana na udanganyifu. Hivyo, tunahakikisha tunajenga msingi wa wataalamu wenye uwezo wa kupambana na changamoto hizi,” alisema.


Aliongeza kuwa katika kongamano hilo, mada mbalimbali zinajadiliwa ikiwemo uchunguzi katika mazingira ya TEHAMA, mbinu za kisasa za kudhibiti udanganyifu katika teknolojia, uchunguzi wa utakatishaji fedha na uadilifu katika manunuzi na miradi ya maendeleo.


Naye Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Sanya, alisisitiza ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ACFE katika kujenga mfumo imara wa uwajibikaji na uadilifu.

“Tumejikita katika kuhakikisha kwamba uwajibikaji na uadilifu vinapewa kipaumbele katika usimamizi wa rasilimali za umma,” alisema.


Kongamano hilo limekutanisha wataalamu wa udhibiti wa udanganyifu kutoka sekta mbalimbali, likiwa na lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za udanganyifu kwa kutumia mifumo ya kisasa.




Ends..

Post a Comment

0 Comments