TARURA KUZIBORESHA BARABARA ZA ARUSHA KWA GHARAMA YA SHILINGI BILIONI 31.5
Na Joseph Ngilisho— Arusha
WAKALA wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Arusha umeahidi kuanza rasmi maboresho ya barabara katika mkoa huo, ikiwemo zile za Jiji la Arusha, kwa kuziba mashimo na kufanya matengenezo ya kiwango cha lami baada ya Serikali kuidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 31.5.
Akizungumza na Arushadigital ofisini kwake mapema leo oktoba 15,2025 ,Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha, Mhandisi Nicolaus Francis, alisema tayari mpango wa matengenezo hayo umeanza, na kwa sasa wako katika hatua ya manunuzi kabla ya utekelezaji kuanza.
> “Jumla ya barabara zenye urefu wa kilometa 13 kutoka wilaya mbalimbali za mkoa huu zitajengwa kwa kiwango cha lami, huku kilometa 206 zikiwa zitajengwa kwa kiwango cha changarawe,” alisema Mhandisi Francis.
Aliongeza kuwa matengenezo ya kawaida ya kuziba mashimo yatatekelezwa kwenye jumla ya barabara zenye urefu wa zaidi ya kilometa 734, ambapo mkataba wake umekamilika na mkandarasi ameshasaini makubaliano ya kuanza kazi.
Hata hivyo, Meneja huyo alilalamikia changamoto kubwa inayotokana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Auwsa), akisema wamekuwa wakiharibu barabara kwa kuchimba mashimo na kuyaacha wazi kwa muda mrefu bila kuyaziba, jambo linalosababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Kuhusu ajali zinazotokana na mwendo kasi wa waendesha pikipiki jijini Arusha, Mhandisi Francis alisema TARURA ina mpango wa kuweka matuta katika maeneo hatarishi, ikiwemo eneo la Sombetini, ambapo hivi karibuni wananchi waliandamana kufuatia kifo cha mwenzao aliyeuawa kwa kugongwa na pikipiki iliyokuwa ikikimbia.
> “Tayari mkandarasi amepatikana na utekelezaji wa ujenzi wa matuta utaanza wiki hii hadi kufikia Jumamosi, ili kudhibiti mwendo kasi wa vyombo vya moto,” alisema.
Mbali na kazi hizo, TARURA imesaini mkataba mwingine wa shilingi bilioni 3.266 kwa ajili ya kutengeneza barabara kuu nne za Jiji la Arusha, ikiwemo Barabara ya Sokoine, Nyerere na Gran Melia, zenye jumla ya urefu wa zaidi ya kilometa 6.
Aidha, Meneja huyo alionya baadhi ya wakandarasi wasio waaminifu wanaoshindwa kukamilisha miradi kwa wakati, akisema hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kuvunjwa kwa mikataba kulingana na taratibu za kisheria.
> “Tumechoka na wakandarasi wasumbufu. Mikataba yetu iko wazi, na kila mkandarasi atawajibika kwa mujibu wa makubaliano kama hatatekeleza miradi kwa wakati,” alisisitiza.
Akihitimisha, Mhandisi Francis aliwataka wananchi wa Arusha kuwa na matumaini, akisema changamoto za barabara mbovu zinakaribia kufika mwisho.
> “Tofauti na ilivyokuwa awali, safari hii fedha zimeidhinishwa na zipo tayari. Wananchi wakae mkao wa kuona mabadiliko makubwa kwenye miundombinu ya barabara za Arusha,” alisema kwa matumaini.
Ends..

0 Comments