Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
WAFANYABIASHARA zaidi ya 400 wa Maduka katika eneo la standi ndogo jijini Arusha wameandamana ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Arusha na kuibua taharuki wakilalamikia kitendo cha halmashauri ya jiji la Arusha kufunga maduka yao kwa makufuri na kusabababisha hasara kubwa.
Kiongozi wa wafanyabiashara hao, dominic Mollel alisema kuwa mapema leo uongozi wa jiji la Arusha wakiongozwa na mwanasheria ,Iddy Ndabhona walifunga maduka ya wafanyabishara kwa madai kwamba wamiliki wa maduka hayo wanadaiwa malimbikizo mbalimbali ya kodi .
"Baada ya kukuta maduka yamefungwa sisi kama viongozi wa wafanyabiashara tuliamua kwenda kuonana na mkuu wa wilaya na baadaye wafanyabiashara wote walitufuata kutaka kujua utaratibu uliotumika kufunga maduka "
Mollel alifafanua kwamba kumekuwepo na msuguano wa muda mrefu baina ya wafanyabishara hao na jiji la Arusha,ambapo jiji la Arusha limetishia kuvunja maduka hayo kwa lengo la kufanya maboresho jambo ambalo limeibua sintofahamu huku wafanyabishara hao wakigomea mikataba mipya inayowatambulisha wao kama wapangaji wa maduka hayo badala ya wajenzi .
Mkuu wa wilaya ya Arusha Joseph Mkude baada ya kuonana na pande zote mbili ofisini kwake, akiwemo kaimu Mkurugenzi wa jiji, Mwanasheria ,mhasibu Mkuu wa jiji ,aliamuru maduka hayo yafunguliwe na wafanyabishara wapewe muda hadi septemba 30,2025 wawe wamelipa madeni yao yanayofikia zaidi ya bilioni 5.
Akiongea na wafanyabishara hao katibu tawala wa wilaya hiyo (Das)Jacob Rombo aliwataka wafanyabishara hao kulipa kodi ya serikali kwa wakati kwani ndio msingi wa maendeleo ya taifa lolote duniani .
Das aliwahakikishia wafanyabishara hao kwamba kwa sasa serikali haina mpango wa kuyavunja maduka hayo ila iwapo mpango huo utatokea watajulishwa ili kuweka utaratibu mzuri wa kuhamia eneo jingine na watapewa kipaumbele cha kurejea baada ya maboresho kukamilika.
"Maagizo ya mkuu wa wilaya ni kwamba kwa sasa maduka yenu hayawezi kuvunjwa ila kama mpango huo utakuja mtashirikishwa na mtapangiwa eneo la kuamishia biashara zetu na maboresho yakimalizika mtapewa kipaumbele kwa mfanyabiashara asiyedaiwa"
Akiongea suala la Mikataba baina ya jiji na wafanyabishara hao ,Das alidai kuwa kwa sasa mkataba huo unapitiwa upya na wanasheria wa msaada wa kisheria wa kampeni ya kisheria ya mama samia lagel aid ili uwe na afya kwa pande zote mbili.
Rombo aliwataka wafanyabishara hao kujiepusha na migomo inayoleta taharuki ikiwemo kufunga barabara,kuandamana ila aliwasihi kutumia busara zaidi kwa kuonana na viongozi wa ngazi ya wilaya au mkoa iwapo kutakuwa na uhitaji huo.
Baadhi ya wafanyabishara hao akiwemo katibu wa wafanyabishara hao Angelus Shokia walimshukuru Mkuu wa wilaya hiyo kwa uamuI wake wakidai kwa sasa watafanyabiashara kwa amani na kuahidi ushirikiano kwa serikali katika ulipaji mapato.
Ends...
0 Comments