WAFANYABIASHARA WAJENZI STEND NDOGO WASHUSHA KILIO KIZITO KWA SERIKALI HATIMA YA MADUKA YAO!

 *KILIO CHA WAWEKEZAJI MADUKA STENDI NDOGO ARUSHA*

MAONI KUHUSU HATMA YA MADUKA YA STENDI NDOGO - JIJI LA ARUSHA.


Kwa heshima na moyo wa uzalendo, sisi wawekezaji maduka stendi ndogo Arusha, tunapenda kutoa kilio na  maoni yetu kwa Serikali kuhusu suala nyeti linalohusu uamuzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuvunja maduka yaliyojengwa katika eneo la Stendi Ndogo Arusha.


Historia inaonesha kuwa maduka haya yalijengwa na wawekezaji binafsi kufuatia makubaliano ya kimaendeleo kati yao na Jiji. Kabla ya ujenzi, eneo hilo lilikuwa makaburi.


 Hata hivyo, Jiji lilikubaliana na wawekezaji kutoa ardhi, huku wao wakigharamia ujenzi kwa fedha zao. Ni muhimu kufahamu kwamba Halmashauri haikuchangia gharama za ujenzi kwa namna yoyote ile.

Tangu wakati huo, kila duka lilikuwa likilipa kodi ya pango ya shilingi 200,000 kwa mwezi, ambayo mwezi Julai 2023 kodi ilipandishwa hadi 250,000 kwa mwezi.


Aidha wafanyabiashara pia hulipa kodi na tozo stahiki kama VAT, Income Tax, Service Levy, gharama za leseni, huduma za maji, usafi, umeme na ulinzi,nk.


Kwa sasa, kuna wawekezaji 400 wanaomiliki maduka hayo kwa kulipa kodi kwa Jiji ya Shs 250,000 kila duka. Biashara hizi zimezalisha ajira kwa watu wengi, huku familia zaidi ya 1,000 (livelihoods) zikitegemea mapato yake kwa maisha ya kila siku. 


Eneo hili limekuwa kitovu muhimu cha uchumi kwa wananchi wa kipato cha kati na cha chini – watu waliowekeza kwa jasho na kujinyima.

Kwa muktadha huo, ni jambo la kusikitisha kuona kwamba Jiji limeamua kubomoa vitega uchumi hivi vya wananchi kwa kigezo cha kuleta maendeleo huku wakipoteza makusanyo ya takribani 1.2 billion  kwa mwaka lakini wakiathiri maisha ya takribani familia 1000. 


Inasemekana Mpango huo unalenga kutumia mabilioni ya fedha kuvunja na kujenga upya, ilhali maeneo mengine muhimu kama Soko Kuu, Soko la Kilombero, Soko la Samunge, na Stendi ya Mkoa bado yako katika hali duni. Kwa mfano, Soko la Samunge bado limejengwa kwa mabanzi – hali inayoharibu taswira ya jiji letu.

Aidha, maeneo kama Kaloleni, Soweto, na Sanawari, ambako nyumba zilizokuwa zinamilikiwa na serikali na Halmashauri ya Jiji zilivunjwa mwaka 2013 kwa lengo la kuwezesha uwekezaji, hadi leo hakuna maendeleo yoyote yaliyofanyika. Wakazi waliokuwa wakiishi katika nyumba hizo walikuwa wapangaji waliolipa kodi ya pango kwa serikali na halmashauri kwa miaka mingi. Hivyo basi, kuvunjwa kwa nyumba hizo kuliwasababishia wananchi hao kupoteza makazi, huku serikali ikipoteza chanzo cha mapato kwa zaidi ya miaka 12 sasa – kwani hakuna uwekezaji wowote uliofanyika katika maeneo hayo.


 Matokeo yake, maeneo hayo yamebaki kuwa mapori yanayotumiwa na wahalifu kujificha – hali inayohatarisha usalama wa wakazi wa maeneo jirani na kuchafua sura ya jiji.


Kwa msingi huu, tunapendekeza kuwa kabla ya kuvunja maduka ya Stendi Ndogo – ambayo yanaingiza mapato na kutoa ajira – Halmashauri ianze kwa kuendeleza maeneo yaliyobomolewa na kutelekezwa kama Kaloleni, Soweto,Faya, Kilombero na Sanawari ili kuongeza vyanzo vya mapato ya kudumu. 


Pia, tunashauri mabilioni yaliyotengwa kwa ajili ya mradi huu yatumike kwanza kuboresha maeneo yenye changamoto kubwa zaidi.


 Halmashauri inapaswa kujikita katika kukusanya kodi na kutoa huduma bora badala ya kujiingiza katika biashara – jambo linaloifanya kuwa mshindani wa sekta binafsi badala ya mwezeshaji, hali inayoongeza urasimu na kuathiri chanzo kikuu cha kodi na ajira.

 

Tunashauri kwamba badala ya kubomoa maduka ambayo tayari yana mchango mkubwa kwa uchumi wa jiji na taifa, nguvu na rasilimali zitumike kuboresha maeneo mengine. Ikiwa lengo ni kuboresha muonekano wa eneo, basi ni vyema wawekezaji waliopo wahusishwe moja kwa moja. Ushirikishwaji huu utaonesha kwamba serikali inaheshimu haki za wamiliki, inatambua mchango wao, na inajenga mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani.


Iwapo maduka haya yatabomolewa, serikali itapoteza mapato, wananchi watapoteza ajira, na jamii itakumbwa na mshtuko wa kiuchumi. Mbaya zaidi, hatua hiyo inaweza kuvuruga imani ya wananchi kwa serikali na kusababisha migogoro isiyo ya lazima kati ya wafanyabiashara na mamlaka hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.


Tunaomba serikali ifikirie upya hatua hii kwa jicho la huruma, haki na busara kwani Wawekezaji hawa ni wajasiriamali wazawa; wengine ni wastaafu,vijana waliomaliza vyuo, wamama ambao wote wanategemea mapato ya maduka haya kuendesha maisha yao ya kila siku ikiwemo kusomesha watoto wao. Ikumbukwe kwamba Walijinyima, wakajenga, lakini sasa wanaishi kwa hofu ya kupoteza kila kitu bila fidia wala maandalizi.


Tunajua Serikali ya Mama Samia inajali na kuheshimu na kusaidia wawekezaji hasa wazawa. Hivyo basi, tunaomba  serikali yetu inayoweka mbele maslahi ya wananchi wake,  inayotambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi, na inayosaidia kuondoa umasikini badala ya kuutengeneza upya iangalie maamuzi ya baraza ka madiwani kwa jicho la tatu.


Maendeleo ya kweli hayawezi kujengwa juu ya maumivu ya wengi. Ni wakati wa kuchagua njia ya hekima  inayolenga maendeleo jumuishi na endelevu,  inayojenga bila kubomoa, inayoinua bila kukandamiza, na inayoshirikisha bila kubagua. 


Serikali yetu sikivu ina nafasi ya kuandika historia ya haki, usawa na matumaini kwa wananchi wake. Tusikose fursa hii muhimu ya kuonesha kwamba tunaweza kusikiliza, kuelewa, na kutenda kwa maslahi mapana kwa wananchi wajasiriamali.

*KAZI IENDELEE*.

Katika Ujenzi wa Taifa, Wawekezaji Stendi Ndogo Arusha.

Post a Comment

0 Comments