Na Joseph Ngilisho ARUSHA
SHIRIKA la Kutetea haki ya wanawake na watoto la MEMUTE ORGANIZATION la jijini Arusha limepinga na kulaani vikali vitendo vya udhalilishaji dhidi ya Rais wa Taifa la Tanzania Samia Suluhu Hassan vinavyofanywa na baadhi ya watu wanaojiita wanaharakati kupitia mitandao ya kijamii .
Akitoa tamko hilo mapema leo Mei 22,2025 katika ofisi za shirika hilo, Mkurugenzi mtendaji wa Memute organization ,Rose Njilo ,alisema wao kama wanaharakati wa haki za binadamu hawakubaliani na vitendo vya baadhi ya watu wanaojiita wanaharakati kutumia mitandao ya kijamii kumdhalilisha rais Samia kwa maneno ya uchochezi .
Hatua hiyo imekuja kufuatia kiongozi wa upinzani Tanzania Tundu Lisu kupandishwa kizimbani Mei 20,2025 huku baadhi ya wanaharakati kutoka nchi jirani waliokuwa wanaingia nchini kufuatilia shauri hilo mahakamani wakizuiwa uwanja wa ndege wa Mwalimu Julias Nyerere, Dar es Salaam na wengine kushikiliwa na polisi kwa mahojiano,na hivyo kuibua kelele za watu wanaojiita wanaharakati mitandaoni.
"Kwa masikitiko makubwa tunalaani video (picha mjongeo) na maandiko yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii yaliyojaa matusi,dhihaka na kejeli za Maksudi dhidi ya Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan "Alisema
Njilo ambaye pia ni mwanamtandao wa kutetea haki za wanawake nchini,alisema kuwa wanaofanya hivyo wanapaswa kutambua kwamba vitendo hivyo havikubaliki kwa taifa lolote na kwamba ni udhalilishaji na ukandamitaji dhidi ya wanawake wote na viongozi Tanzania .
"Wakumbuke kwambà sisi Watanzania tumekuwa mstari wa mbele kudumisha heshima baina ya mataifa haya ndugu Hatujawahi kutumia mitandao ya kijamii kudhalilisha na kutukana viongozi wetu "
"Inashangaza kuona mtu anayejitambulisha kama mtetezi wa haki za binadamu na kushindwa kumtambua Rais kama binadamu mwenye haki ,utu ,heshima na dhamana kubwa ya kitaifa na kimataifa na kuamua kumpaka matope na kwamba kitendo hicho si tu ni udhalilishaji wa mtu bali ni kuvunja heshima ya Taifa zima la Tanzania"Alisema.
Njilo aliwataka wanaharakati wa haki za wanawake na haki za kibinadamu kuungana kwa pamoja na kukemea udhalilishaji wa aina yoyote dhidi ya viongozi wanawake.
"Tunahimiza waandishi wa habari, watumiaji wa mitandao ya kijamii kuwa mabalozi na siyo kuchochea chuki ,ukatili wa kijinsia au Matusi dhidi ya viongozi wa nchi"
Naye Mkurugenzi wa shirika la Dunia Salama Foundation,Iddy Ninga na mwanamtandao wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto Tanzania , alisema kitendo cha udhalilishaji kwa Kiongozi wa nchi aliyeaminiwa na wananchi wake hakikubaliki na wao kama watetezi wa haki za binadamu amezishauri nchi wanachama wa jumuiya ya afrika mashariki (EAC)kuangalia njia sahihi ya kukomesha vitendo vya aina hiyo .
"Tunaitaka nchi husika ambayo ni mwanachama wa jumuiya ya afrika mashariki,Kuwakanya wananchi wake na kuwazuia kuendelea kumdhalilisha rais wetu na kuendelea kuwadhalilisha wasanii wa Tanzania kwani watanzania hatuna tabia ya kutukana viongozi wetu"
Aidha mkurugenzi huyo ameliomba bunge la Tanzania kujadili kwa kina hali hiyo na kutoa tamko linaloweza kusaidia kukomesha vitendo vya aina hiyo vinavyolenga kulidhalilisha Taifa la Tanzania na Rais wake.
Ends.....
0 Comments