MWANAHARAKATI WA KENYA BONIFACE MWANGI APATIKANA

By arushadigtal

 

Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi ameachiliwa huru na Tanzania, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Haki Afrika aliiambia BBC.


Hussein Khalid alithibitisha kuwa alikuwa pamoja na Mwangi wakiwa njiani kutoka Mombasa na sasa wanaelekea Nairobi.


Waziri Mkuu na Katibu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi, awali alikuwa pia ametangaza kuachiliwa kwa mwanaharakati huyo karibu na eneo la mpaka kati ya nchi hizo mbili ambaye alikuwa amekamatwa nchini Tanzania kwa siku kadhaa.

Awali, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Kenya ilisema kuwa "licha ya maombi kadhaa ya kumuona mwanaharakati huyo, maafisa wa Serikali ya Kenya hawakuwezeshwa kumfikia wala kuwa na habari zozote kumhusu Bw Mwangi."


Wizara hiyo pia ilionyesha wasiwasi juu ya afya yake na kukosekana kwa habari kuhusu kuzuiliwa kwake," ilisema.


Kenya ilitoa wito kwa serikali ya Tanzania kuchukua hatua ya "haraka na bila kuchelewa" ili kuwezesha ufikiwaji wa kibalozi au kuachiliwa kwa Mwangi, kwa mujibu wa sheria na kanuni za kimataifa kidiplomasia.


Mwanaharakati Boniface Mwangi na Agather Atuhaire wa Uganda walizuiliwa nchini Tanzania mapema wiki hii nchini Tanzania, ambao walikuwa wameenda kuhudhuria kesi ya kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu.


Hapo jana, Njeri Mwangi, mkewe Boniface Mwangi aliandamana na mwanawe mkubwa, mama yake na mawakili wake hadi katika ubalozi wa Tanzania nchini Kenya na baadaye kuelekea katika Wizara ya Mambo ya Nje mjini Nairobi, kuelezea hofu kubwa kuhusu hali ya mume wake akitaja kuwa hajazungumza naye tangu Jumatatu alipokamatwa.


"Alikuwa amekwenda kumjulia Agatha katika kituo cha polisi cha central kule Tanzania na akanipigia simu. Punde simu yake ikakatika na nadhani ni hapo ilipochukuliwa. Lakini si kawaida yake, angekuwa amefanya kila awezalo kupata njia ya kuwasiliana na mimi. Ila ni kimya tu. Kwa hivyo nina wasiwasi kwa sababu sijui kama hajiwezi, ameumia au yuko vipi," Alisema Njeri.


Mudavadi, katika taarifa yake, alisema Mwangi aliachiliwa huru Alhamisi asubuhi na mamlaka ya Tanzania baada ya serikali kuingilia kati.


Hata hivyo, hakuna taarifa zozote zilizotolewa kuhusu hali yake ya afya hadi kufikia sasa.

Ends...

Post a Comment

0 Comments