MAKAMU WA RAIS DKT MPANGO AIPA TANO BENKI YA CRDB,AITAKA KUTILIA MKAZO TISHIO LA UHALIFU WA KIMTANDAO ILI KIJENGA IMANI KWA WATEJA.

 Na Joseph Ngilisho- ARUSHA 


MAKAMU wa Rais  Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Benki ya CRDB kuweka mkazo zaidi katika udhibiti wa tishio la uhalifu wa kimtandao ili kujenga imani ya wateja na kulinda heshima ya benki hiyo. 

Aidha alisema Benki ya CRDB haina budi kujihami mapema na wakati wowote kwa sababu, kukua kwa matumizi ya teknolojia kumeleta wimbi la matukio ya uhalifu wa kimtandao unaohatarisha mitaji ya benki duniani na kuongeza gharama za kukabiliana nao.


Dkt Mpango ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB inayoenda sanjari ma Maadhimisho ya Miaka 30 ya Benki ya CRDB ,katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).


Alisema matumizi makubwa ya teknolojia yanaondoa mipaka ya kijiografia na hivyo kuunganisha huduma za fedha duniani hivyo ni muhimu kuwepo na menejimenti ya vihatarishi na hitaji la kuzingatia kanuni za kifedha za kimataifa.


Alisema ni vema kuendelea kufanya mageuzi ya kiteknolojia kwa kuongeza matumizi ya huduma za kimtandao ili kuongeza ufanisi, usalama, na ushindani. 




 Aliwasihi kufanya ushirikiano  na wadau wa teknolojia ya fedha ili kubuni bidhaa na huduma zenye ubora. Amesema kuwekeza kwenye Teknolojia kutapunguza gharama za uendeshaji, kuwafikia wateja wengi zaidi kwa muda mfupi hususan walio vijijini na maeneo yasiyo na matawi na kwa watu wenye kipato cha chini au wasioweza kufungua akaunti za kawaida.

Katika kulinda mazingira, Makamu wa Rais ametoa rai kwa mabenki kuangalia uwezekano wa kuunganisha nguvu kwa kuwa na miradi ya pamoja na Taasisi nyingine za fedha, ili kupata kiwango kikubwa zaidi cha fedha na kuziba pengo la ufadhili wa miradi ya mazingira ambalo bado ni kubwa mno. 


Makamu wa Rais alisema Serikali imejizatiti kuhakikisha kuwa sekta ya fedha inaendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi. Amesema Serikali imeboresha sera na kuweka mifumo madhubuti, imejenga miundombinu wezesha na imeendelea kukuza uchumi wa nchi na kipato cha wananchi.

Pia alisema serikali ilipitisha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ili kuweka msingi imara wa kisheria kwa uendeshaji wa benki na taasisi nyingine za kifedha nchini.

 Kadhalika, alisema serikali imetengeneza sera mbalimbali zikiwemo,  Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2000,  Mpango wa Taifa wa Huduma  Jumuishi za Fedha  (Awamu ya Kwanza 2014-2016, Awamu ya Pili 2018-2022 na Awamu ya Tatu 2023-2028), Mpango wa Taifa wa Elimu ya Fedha (2016-2020), Programu ya Kutoa Elimu ya Fedha kwa Umma (2021/22 – 2025/26),  Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha  ya mwaka 2017, Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (2020/21 -2029/30) pamoja  na Sheria ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018. 

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda alisema Serikali imepokea kwa furaha ujenzi wa shule ya sekondari ya mfano itakayojengwa na Benki ya CRDB katika Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam ambayo pamoja na ubora wa miundombinu ya ufundishaji inayotarajiwa kuwa dira kwa shule zingine za umma na binafsi. Amesema zawadi hiyo ni ya kipekee kutoka kwa benki kwenda kwa jamii. 

Prof. Mkenda ameihakikishia Benki ya CRDB kwamba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaendelea kushirikiana kwa karibu na benki hiyo kwa maslahi ya Taifa na kwa maendeleo ya Elimu kwa mustakabali wa vizazi vya sasa na vijavyo.  

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay ameishukuru Serikali, wadau, wanahisa, wateja, washirika kwa kuendelea kuiamini Benki ya CRDB na kushirikiana katika kipindi cha miaka 30. Amesema miaka 30 iliyopita imekuwa na mafanikio makubwa na wanatarajia kuifikisha banki hiyo katika viwango vya juu zaidi.

Dkt. Laay alisema Benki ya CRDB itaendelea kuwa mshiriki namba moja wa maendeleo kwa Serikali, wadau wa maendeleo pamoja na wateja wote. 

Awali akitoa taarifa ya historia na maendeleo ya Benki ya CRDB, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Abdulmajid Nsekela amesema katika kipindi cha miaka 30 Benki hiyo imefanya mageuzi makubwa na kuwa benki mwanzilishi wa huduma mbalimbali za kifedha nchini. Ameongeza kwamba Benki imeendelea kubuni huduma mahususi kwa makundi mbalimbali kwa kuzingatia idadi kubwa ya wanawake na vijana ambao wapo katika sekta isiyo rasmi. 

Alisema mwaka 2019 CRDB  ilikuwa Benki ya kwanza Afrika mashariki na kati kusahiliwa na shirika kubwa duniani la mazingira la GCF na kupewa daraja la kati kusimamia miradi yenye kiwango cha zaidi ya dola milioni 200.

Nsekela alisema Benki hiyo inajivunia kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa sera za mazingira, jamii na utawala bora.





Ends...


Post a Comment

0 Comments