VIATARISHI VYA DUNIA VYATAJWA KUTISHIA UCHUMI WA TANZANIA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
TANZANIA imetakiwa kuimarisha mifumo ya tahadhari na udhibiti wa viatarishi vya kiuchumi ili kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na vita vya kimataifa, kupanda kwa bei ya mafuta na kuvurugika kwa minyororo ya usambazaji wa bidhaa, huku mvutano katika Mlango-Bahari wa Hormuz ukitajwa kuwa miongoni mwa vitisho vinavyoweza kuongeza gharama za maisha nchini.Serikali imesema misukosuko inayotokea katika maeneo mbalimbali duniani inaweza kuathiri uchumi wa Tanzania hata kama nchi haishiriki moja kwa moja katika migogoro hiyo, kutokana na utegemezi wa biashara ya kimataifa, uagizaji wa mafuta, malighafi na bidhaa nyingine muhimu.
Kauli hiyo imetolewa jijini Arusha jana, Novemba 16, 2026, na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, akifungua mkutano mkuu wa tisa wa mwaka wa Taasisi ya Usimamizi wa Viatarishi Tanzania (IRMT), uliowakutanisha wataalamu wa usimamizi wa viatarishi kutoka sekta ya umma na binafsi.Mwandumbya alisema vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati na changamoto za usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz vinapaswa kufuatiliwa kwa karibu kwa sababu kuvurugika kwa njia hiyo kunaweza kusababisha kupanda kwa bei ya nishati, kuongeza gharama za usafirishaji na uzalishaji na hatimaye kuathiri maisha ya wananchi.
Alisema uzoefu wa majanga yaliyopita, ikiwemo janga la COVID-19 na vita vya Urusi na Ukraine, umeonesha kuwa misukosuko ya kimataifa inaweza kusababisha madhara makubwa kwa uchumi wa ndani, hata pale nchi husika inapokuwa mbali na eneo la tukio.
Alitolea mfano janga la COVID-19 lililoukumba ulimwengu kuanzia mwaka 2019, ambalo lilikwamisha shughuli nyingi za kiuchumi na kuchelewesha utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini, ikiwemo baadhi ya shughuli za ujenzi wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere kutokana na changamoto za upatikanaji wa mashine zilizokuwa zikizalishwa nchini China.
Alisema vita vya Urusi na Ukraine navyo vilisababisha misukosuko katika upatikanaji wa bidhaa muhimu kama mafuta, mbolea na ngano, hali iliyochangia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na bidhaa katika masoko ya kimataifa.
“Bidhaa hizo zinapopanda bei, zinaathiri uwezo wa wananchi wetu kununua mahitaji yao. Hapo Serikali inapaswa kuwa na mikakati ya kuingilia kati ili kuhakikisha madhara hayo hayaangukii kwa wananchi wa kawaida,” alisema.
Alisema Tanzania inapaswa kujenga uwezo wa kutambua viatarishi kabla havijatokea na kuweka mikakati ya kukabiliana navyo badala ya kusubiri madhara yajitokeze ndipo hatua za dharura zianze kuchukuliwa.
Akizungumzia uimara wa uchumi wa Tanzania, Mwandumbya alisema nchi ina akiba ya fedha za kigeni inayoweza kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi cha miezi 4.3, kiwango kinachozidi kiwango cha chini cha miezi minne.
Alisema hali hiyo ni miongoni mwa viashiria vya uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya nje, lakini bado kuna umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa viatarishi katika taasisi za umma na binafsi.
Aliwataka maafisa wanaosimamia eneo hilo kuhakikisha wanatoa ushauri wa kitaalamu kwa wakati, wanabaini changamoto zinazoweza kuathiri taasisi na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kuzidhibiti.
Alisema usimamizi madhubuti wa viatarishi ni muhimu katika kulinda rasilimali, kuongeza ufanisi wa taasisi na kuhakikisha mipango ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati.
Pia aliwataka wafanyabiashara na wawekezaji katika sekta za madini, utalii, kilimo na biashara kufanya tathmini ya viatarishi kabla ya kufanya maamuzi ya uwekezaji, wakizingatia mabadiliko ya bei, upatikanaji wa bidhaa na gharama za uzalishaji.
Alisema mifumo hiyo ni muhimu pia katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa dola trilioni moja
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa IRMT, Christopher Njovu, alisema taasisi nchini zinapaswa kujiandaa kukabiliana na viatarishi vinavyotokana na mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya teknolojia na migogoro ya kivita duniani, ambavyo vinaweza kuvuruga shughuli za taasisi na kudhoofisha ukuaji wa uchumi.
Alisema mkutano huo umejikita katika maeneo makuu matatu ambayo ni kubadilishana uzoefu wa kitaalamu, kuongeza maarifa na elimu kwa wadau pamoja na kuimarisha uwezo wa wataalamu katika kusimamia viatarishi vinavyojitokeza katika mazingira ya kazi na uwekezaji.
Akizungumzia mabadiliko ya tabianchi, Njovu alisema taasisi zinapaswa kujipanga mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwemo matukio ya mvua kubwa na ukame
Alitolea mfano tahadhari zinazotolewa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa El Niño, akisema ni muhimu taasisi kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kujiandaa ili athari zake zisiathiri shughuli za kiuchumi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Alisema eneo jingine linalohitaji umakini ni usalama wa mifumo ya kidijitali (cybersecurity), kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia katika shughuli za kifedha na utoaji wa huduma.
Alisema pamoja na teknolojia kurahisisha shughuli mbalimbali, matumizi yasiyo salama yanaweza kusababisha upotevu wa fedha, taarifa muhimu na rasilimali za taasisi.
“Kwa sasa huwezi kukwepa suala la teknolojia. Maisha mengi yanaendeshwa kupitia mitandao, lakini tunapaswa kuhakikisha mifumo yetu iko salama ili kulinda rasilimali fedha na taarifa,” alisema.
Alisema migogoro ya kivita duniani nayo ni changamoto inayopaswa kupewa kipaumbele kwa sababu inaweza kuvuruga minyororo ya upatikanaji wa malighafi, kuongeza gharama za uzalishaji na kupandisha bei za bidhaa muhimu.
Njovu alisema taasisi zinapaswa kujenga utamaduni wa kusimamia viatarishi katika mipango na maamuzi yao ya kila siku, badala ya kusubiri majanga yatokee ndipo zianze kutafuta suluhisho.
Alisema kupitia mkutano huo, wadau wanatarajiwa kupata maarifa na uzoefu utakaosaidia kuimarisha mifumo ya usimamizi wa viatarishi na kuhakikisha changamoto za ndani na nje ya nchi hazikwamishi utekelezaji wa malengo ya taasisi na ukuaji wa uchumi wa taifa.
Ends




Post a Comment