LUKUMAY AUNGA MKONO MPANGO WA KUREJESHA MASHAMBA YA MAUA
....Ataja hatua hiyo kuwa fursa ya kufungua ajira kwa vijana na wanawake, kuongeza uzalishaji wa mboga na matunda na kukuza uchumi wa Arusha.
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Dkt Lukumay alisema kurejeshwa kwa mashamba hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya kilimo, hususan uzalishaji wa mboga mboga na matunda kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Alisema mpango huo una umuhimu mkubwa kwa Mkoa wa Arusha, ambao una mazingira na uwezo wa kuendeleza kilimo cha bustani, huku uwekezaji katika mashamba hayo ukiweza kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Akizungumza Nov,09,2026 katika jukwaa la HortiLogistica Africa linalofanyika katika viwanja vya TGT, nje kidogo ya Jiji la Arusha, Dkt Lukumay alisema kurejeshwa kwa mashamba hayo kunapaswa kupewa kipaumbele ili kuongeza maeneo ya uzalishaji na kuwashirikisha wananchi katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya kilimo.
Jukwaa hilo limefunguliwa na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, likiwakutanisha wadau wa kilimo, wawekezaji, wataalamu na wafanyabiashara wa mazao ya bustani kutoka maeneo mbalimbali.
Alisema Serikali inapochukua hatua ya kurejesha mashamba hayo katika uzalishaji, ni muhimu pia kuweka mazingira yatakayowawezesha vijana na wanawake kushiriki katika shughuli za uzalishaji, uchakataji, ufungashaji na biashara ya mazao.
Dkt Lukumay alisema fursa hiyo inaweza kusaidia kuongeza ajira, kipato cha kaya na mapato ya Taifa kupitia uzalishaji wa mazao yenye ubora na yanayokidhi viwango vya masoko ya kimataifa.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa wakulima kutumia teknolojia za kisasa, kupata elimu ya kilimo bora na kuimarisha uhusiano na wanunuzi ili kuhakikisha mazao yanayozalishwa yanapata masoko ya uhakika.
Alisema Arusha ina nafasi ya kuimarisha zaidi hadhi yake katika uzalishaji na biashara ya mazao ya bustani endapo juhudi za Serikali, sekta binafsi na wakulima zitaunganishwa.
Aliongeza kuwa jukwaa la HortiLogistica Africa ni fursa ya kujenga ushirikiano wa kibiashara na kiteknolojia utakaosaidia wakulima kupata masoko mapya na kuongeza thamani ya mazao yao.
Ends

Post a Comment