MCHIMBAJI MDOGO GEITA AIBUA AJENDA YA WACHIMBAJI, ATAMANI KUPANDA DARAJA
Aeleza namna maonesho ya madini yalivyomfungulia milango ya wawekezaji, teknolojia na mitaji
Na Joseph Ngilisho | DAR ES SALAAM
MCHIMBAJI mdogo wa madini ya dhahabu kutoka mkoani Geita, Omary Kamage, ameibua matarajio ya wachimbaji wadogo nchini kupanua shughuli zao na kupanda kutoka uchimbaji mdogo kwenda uchimbaji wa kati na hatimaye kuwa wawekezaji wakubwa katika sekta ya madini, akitaja upatikanaji wa mitaji, teknolojia na maarifa kuwa nguzo muhimu ya kufanikisha azma hiyo.
Omary Kamage, kupitia kampuni yake ya Kamage Investments inayojihusisha na uchimbaji wa dhahabu, alisema ushiriki wake katika maonesho ya sekta ya madini jijini Dar es Salaam umekuwa fursa muhimu ya kujifunza, kutafuta wawekezaji na kujenga mahusiano ya kibiashara yanayoweza kubadilisha kiwango cha shughuli zake za uchimbaji.
Alisema wachimbaji wengi wadogo wana uwezo na dhamira ya kukuza shughuli zao, lakini wanahitaji kuunganishwa na mifumo ya kiteknolojia, mitaji na wadau wenye uwezo wa kuwasaidia kuvuka hatua ya uchimbaji mdogo.
Alisema maonesho hayo yamefungua fursa ya kukutana na kampuni na wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali, ambao wameonesha nia ya kushirikiana na wachimbaji wenye mipango ya kupanua shughuli zao.
“Tumetoka kwenye uchimbaji mdogo, lakini tunatamani kuingia kwenye uchimbaji wa kati. Ndiyo maana tumesafiri kutoka Geita mpaka Dar es Salaam kuja kujifunza na kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya madini,” alisema Kamage.
Aliongeza: “Tumekutana na watu mbalimbali ambao wameonesha nia ya kuwekeza katika kampuni zetu. Mtu anakutana na wewe na kukuuliza unahitaji mtaji wa kiasi gani ili uweze kuendelea na shughuli zako. Hizi ni fursa ambazo tunazihitaji sana.”
TEKNOLOJIA YAIBUA MATUMAINI
Kamage alisema miongoni mwa mambo yanayowavutia wachimbaji wadogo katika maonesho hayo ni teknolojia mbalimba.li zinazotumika katika uchimbaji na uchakataji wa madini, ambazo zinaweza kuwasaidia kuongeza ufanisi na kupanua uzalishaji.
Alitaja teknolojia ya CIP kuwa miongoni mwa maeneo wanayojifunza kutoka kwa wadau wa sekta hiyo, akieleza kuwa maarifa ya teknolojia za kisasa ni muhimu kwa wachimbaji wanaotaka kubadilisha kiwango cha shughuli zao.
Alisema lengo lao si kuendelea kufanya shughuli za uchimbaji kwa mazoea, bali kujifunza mifumo mipya itakayowawezesha kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi na kufikia viwango vya juu vya uwekezaji.
“Tunazidi kujifunza hapa kuhusu mambo mbalimbali yanayohusiana na uchimbaji na uchakataji wa madini. Tunataka kutoka kwenye uchimbaji mdogo na kwenda uchimbaji wa kati, hivyo lazima tujifunze teknolojia na mifumo inayotumika katika hatua hiyo,” alisema.
SAFARI YA GEITA HADI DAR ES SALAAM
Akieleza sababu za kusafiri kutoka Geita kushiriki maonesho hayo, Kamage alisema mafanikio ya wachimbaji wadogo hayawezi kutegemea shughuli za migodini pekee, bali pia uwezo wa kutafuta maarifa, kujenga mahusiano na kutumia fursa zinazojitokeza nje ya maeneo yao ya uchimbaji.
Alisema kukutana ana kwa ana na kampuni zinazotoa huduma za migodi, wawekezaji na wadau wa teknolojia kunawapa nafasi ya kuelewa mahitaji ya soko na fursa za kushirikiana katika kukuza biashara zao.
Kwa mujibu wa Kamage, wachimbaji wadogo wanapaswa kuyatumia majukwaa kama hayo si kwa kutembelea mabanda pekee, bali kuhakikisha wanapata maarifa na mawasiliano yatakayowasaidia wanaporejea kwenye maeneo yao ya kazi.
AIPONGEZA WIZARA YA MADINI
Katika hatua nyingine, Kamage aliipongeza Wizara ya Madini chini ya Waziri Anthony Mavunde kwa kuwawezesha wachimbaji wadogo kushiriki katika majukwaa ya kukutana na wadau wa ndani na nje ya nchi.
Alisema ushiriki wa wachimbaji wadogo katika maonesho hayo ni fursa ya kujifunza na kuwasilisha mahitaji yao kwa wadau wanaoweza kusaidia kukuza shughuli zao.
“Tunampongeza Waziri wa Madini, Anthony Mavunde. Hata sisi wachimbaji wadogo kupata nafasi ya kushiriki katika maonesho haya ni fursa kubwa,” alisema.
WITO KWA VIJANA: MSIKATE TAMAA
Kamage alitumia nafasi hiyo kutoa ujumbe kwa vijana wanaotaka kuingia katika shughuli za ujasiriamali na uchimbaji wa madini, akiwataka kuwa wavumilivu, wenye nidhamu na wasiokata tamaa wanapokutana na changamoto.
Alisema mafanikio katika shughuli za kiuchumi yanahitaji kujituma na kupambana kutoka hatua ya chini, hivyo vijana wanapaswa kuwa na malengo na kuyafanyia kazi badala ya kusubiri mafanikio ya haraka.
“Kikubwa ni kupambana kama tunavyopambana sisi. Tumeanzia sifuri mpaka hapa tulipofikia. Vijana wasikate tamaa, wapambane, wawe na nidhamu na wamtegemee Mungu,” alisema.
ANATARAJIA KUWASILISHA MAONI SERIKALINI
Kamage alisema wana matarajio ya kutumia majukwaa ya maonesho hayo kuwasilisha maoni yao kwa Serikali kuhusu namna ya kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogo na kuwawezesha kufikia viwango vya juu vya uzalishaji na uwekezaji.
Alisema wanatarajia kupata nafasi ya kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuwasilisha maoni na matarajio yao, akieleza kuwa ni muhimu sauti za wachimbaji wadogo kusikilizwa katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya sekta hiyo.
Alisisitiza kuwa wanataka maoni hayo yafanyiwe kazi ili kuongeza fursa za mitaji, teknolojia na ushirikiano kati ya wachimbaji wadogo na wawekezaji wakubwa.
Alisema lengo lake ni kurejea Geita akiwa na maarifa mapya, mahusiano ya kibiashara na fursa zitakazosaidia kampuni yake ya Kamage Investments kuvuka kutoka uchimbaji mdogo kwenda uchimbaji wa kati.
MWISHO


Post a Comment