Ad
Breaking🔥

ATC YATAKIWA KUZALISHA WAHANDISI WATAKAOBADILI UCHUMI WA TAIFA

 ATC YATAKIWA KUZALISHA WAHANDISI WATAKAOBADILI UCHUMI

..Dkt Salukele, Mbonde wataka wahitimu 1,337 wawe wabunifu, wazalishaji wa teknolojia na watengeneza ajira; Teaching Factory kufikia asilimia 98

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA 

CHUO cha Ufundi Arusha (ATC) kimetakiwa kuimarisha mafunzo ya vitendo, utafiti na ubunifu ili kuzalisha wahandisi na wataalamu watakaoweza kutatua changamoto za jamii, kuanzisha ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania unaotegemea viwanda na teknolojia.

Wito huo umetolewa Nov,12,2026 katika Mahafali ya 18 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Arusha, ambapo jumla ya wahitimu 1,337 walitunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo ya ufundi.

Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt Fredrick Salukele, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Ndomba, alisema elimu ya ufundi siyo chaguo la pili, bali ni msingi muhimu wa kujenga uchumi imara unaotegemea teknolojia, viwanda na rasilimali watu wenye ujuzi.

Alisema maendeleo ya Tanzania yanahitaji wataalamu wenye uwezo wa kubuni, kujenga, kuendesha, kukarabati na kutunza mifumo mbalimbali inayowezesha uzalishaji na utoaji wa huduma.


“Tunapozungumzia maendeleo ya nchi, tunazungumzia pia watu wenye uwezo wa kubuni, kujenga, kuendesha, kukarabati na kutunza mifumo inayowezesha maendeleo hayo,” alisema.

Alisema ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ATC inapaswa kuhakikisha mitaala yake inaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira, hususan katika sekta za viwanda, nishati, maji, afya, ujenzi na huduma za kidijitali.

Alikitaka chuo hicho kushirikiana zaidi na waajiri katika kuboresha mitaala, kuongeza mafunzo ya vitendo na kupima mafanikio yake kwa kuangalia uwezo wa wahitimu kujiajiri, kuajiriwa na kuchangia uzalishaji.

Katika hatua nyingine, Dkt Salukele alisema ujenzi wa kiwanda cha mafunzo na uzalishaji (Teaching Factory) cha ATC umefikia asilimia 98, huku mashine na vifaa kutoka Austria vikitarajiwa kuwasili mwishoni mwa Novemba mwaka huu.

Alisema uwekezaji huo utabadilisha mfumo wa mafunzo kwa kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa kutumia mashine halisi za viwandani, kuzitumia kwa usalama na kuzalisha bidhaa na huduma zenye viwango.

Alisisitiza kuwa kiwanda hicho kinapaswa kuwa daraja linalounganisha darasa, karakana na soko la ajira, huku akitaka chuo kuhakikisha maandalizi ya uendeshaji, matengenezo ya vifaa, usalama na mafunzo ya wakufunzi yanafanyika mapema.

Akizungumzia Kampasi ya Kikuletwa, Dkt Salukele alisema ATC inaandaa kituo cha mafunzo na uzalishaji wa nishati jadidifu chenye uwezo wa kuzalisha megawati 1.65 za umeme.

Alisema mradi huo wenye thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 20.25 unahusisha ujenzi wa bwawa la kuhifadhi maji na ukarabati wa mifereji.

Alisema kituo hicho kinatarajiwa kuwa zaidi ya eneo la kuzalisha umeme, kwa kuwa kitatoa fursa za mafunzo, utafiti na ubunifu wa teknolojia za nishati safi kwa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki.

Kuhusu sekta ya afya, alisema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya chuo hicho inayotarajiwa kuanza kutoa huduma Januari 2027.

Alisema hospitali hiyo ina nafasi ya kuwa kituo muhimu cha uhandisi wa vifaa tiba nchini, kwa kuunganisha huduma za afya, mafunzo kwa vitendo, utafiti na uwezo wa ndani wa kutengeneza na kutunza vifaa tiba.

Alitaja ushirikiano na taasisi za kimataifa zikiwamo Beta International, Cornell University na Clemson University kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha utaalamu wa ndani na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje.

Pia aliipongeza ATC kwa ubunifu wa mita za maji za malipo ya awali na ushirikiano wake na Hans Paul Group kupitia mradi wa E-Motion unaohusu teknolojia ya magari ya umeme, pamoja na vyuo vikuu vya Hanyang cha Korea Kusini na Hanze cha Uholanzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Utawala ya ATC, Noel Mbonde, alisema chuo hicho kinapaswa kujielekeza zaidi katika kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kutengeneza ajira, kubuni teknolojia na kutoa suluhisho kwa changamoto za kiuchumi na kijamii.

Alisema mafanikio ya taasisi za elimu hayawezi kupimwa kwa idadi ya majengo na miradi inayotekelezwa pekee, bali kwa ubora wa wahitimu, teknolojia zinazozalishwa, ubunifu na mchango wa taasisi hizo katika kukuza uchumi wa taifa.

Alisema uwekezaji unaofanyika ATC unapaswa kuonekana katika uwezo wa wahitimu kutumia maarifa yao kubuni bidhaa, kuboresha huduma na kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali.


Naye Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha, Profesa Mussa Chacha, aliziomba taasisi za Serikali, mashirika ya umma na hasa sekta binafsi kuwapa kipaumbele wahitimu hao kwa kuwapatia nafasi za ajira na kujenga uzoefu wa kazi.

Alisema wahitimu hao wamepata maarifa, ujuzi, umahiri na nidhamu zinazohitajika katika soko la ajira, hivyo wanapaswa kuaminiwa na kupewa nafasi ya kuonyesha uwezo wao.

“Ninaomba mashirika ya umma, taasisi za Serikali, jamii ya Watanzania na zaidi sekta binafsi wawapokee vijana wetu na kuwapa fursa za kuendeleza maisha yao. Ujuzi mnao, maarifa mnayo, umahiri mnao na nidhamu mnayo,” alisema.

Alisema wahitimu hao ni sehemu ya nguvu kazi inayohitajika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi shindani unaotegemea viwanda na teknolojia.

Profesa Chacha alisema ATC pia imepanua wigo wa mafunzo kwa kuwajumuisha vijana waliojifunza ufundi kwa vitendo mitaani wakiwa wasaidizi wa mafundi, lakini hawakuwa na nafasi ya kupata mafunzo rasmi.

Alisema kupitia ushirikiano na wadau, wakiwamo Chama cha Wakandarasi na Watoa Huduma Washirika Tanzania (TUKASA), vijana hao wamepata fursa ya kuongeza ujuzi na kuboresha viwango vya kazi zao.

Alisema kundi hilo lina umuhimu mkubwa kwa kuwa baadhi yao walishiriki katika ujenzi wa majengo mengi nchini, lakini sasa wanapata nafasi ya kuongeza maarifa na umahiri kupitia mafunzo rasmi.

Kwa mujibu wa Profesa Chacha, kati ya wahitimu 1,337, wahitimu 444 ni wa shahada, 45 shahada za uzamili, 660 stashahada, tisa stashahada ya juu, 16 stashahada ya awali na 163 wa mafunzo ya ufundi stadi.

Alisema chuo kitaendelea kuwa karibu na wahitimu hata baada ya kumaliza masomo, ikiwamo kuwapatia fursa za kuongeza ujuzi kupitia Teaching Factory bila malipo.


Katika maelekezo yake, Dkt Salukele alisisitiza umuhimu wa kuongeza fursa kwa wasichana na wanawake kujiunga na kuendelea na masomo ya sayansi, teknolojia na uhandisi.

Alisema pia ATC inapaswa kuimarisha mfumo wa kufuatilia wahitimu wake ili kubaini wanaoajiriwa, wanaojiajiri na namna wanavyotumia ujuzi walioupata kuchangia uzalishaji.

Akizungumza na wahitimu, aliwataka kutosubiri ajira pekee, bali kutumia maarifa yao kutambua changamoto zilizopo katika jamii na kuzigeuza kuwa fursa za kiuchumi.

Msingoje kila fursa ije ikiwa tayari imeandaliwa. Fursa nyingine zinatokana na wewe mwenyewe kwa kuangalia changamoto zilizopo kwenye jamii na kujiuliza unaweza kutengeneza nini,” alisema.

Alisema wahitimu wana nafasi ya kubuni suluhisho katika sekta za maji, nishati na afya ambazo zinahitaji teknolojia na wataalamu wenye ujuzi.

Aliongeza kuwa kuhitimu si mwisho wa safari ya kujifunza, bali ni mwanzo wa kuthibitisha thamani ya elimu waliyoipata kupitia kazi, ubunifu na mchango wao kwa jamii.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post