LUGANGIRA USO KWA USO NA BODABODA ATANGAZA OPERESHENI KABAMBE
...Atatembea kijiwe kwa kijiwe, ataka kila dereva awe na kitambulisho chenye QR Code
Aahidi samani za ofisi ya umoja, Chung’ong atangaza kuwa Balozi wa Arumeru
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MKUU wa Wilaya ya Arumeru, Neema Kichiki Lugangira, ametangaza operesheni maalumu ya kuwatambua waendesha bodaboda wote wilayani humo, akiwataka wananchi kuepuka kutumia huduma za madereva wasiotambulika ili kuimarisha usalama na kudhibiti uhalifu.Lugangira amesema operesheni hiyo itahusisha Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, huku kila dereva akitakiwa kutambulika na uongozi wa eneo lake kabla ya kuruhusiwa kufanya shughuli za usafirishaji wa abiria kwa pikipiki.
Akizungumza leo Jumanne, Oktoba 13, 2026, wakati wa uzinduzi wa ofisi za Umoja wa Waendesha Bodaboda wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Lugangira alisema madereva watatakiwa kuwa na vitambulisho maalumu pamoja na mavazi yenye msimbo wa QR (QR Code), utakaosaidia kurahisisha utambuzi wao.
Alisema hatua hiyo inalenga kuwatenganisha waendesha bodaboda wanaofuata sheria na watu wanaotumia shughuli hiyo kujihusisha na uhalifu, ambao kwa kiasi fulani huathiri taswira ya kundi hilo.
“Tunataka kila mwendesha bodaboda atambulike na uongozi wa eneo lake. Wananchi pia wanapaswa kupewa elimu ili wajue umuhimu wa kutumia huduma za madereva wanaotambulika,” alisema.
Lugangira aliwataka waendesha bodaboda kuwa sehemu ya mfumo wa ulinzi wa jamii kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu, akisisitiza umuhimu wa nidhamu, weledi na uzingatiaji wa sheria katika kazi zao.
Alisema Serikali inatambua mchango wa waendesha bodaboda katika shughuli za kiuchumi na usafirishaji, hivyo ofisi yake iko tayari kushirikiana nao kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.
Pia aliwahimiza vijana hao kutumia fursa za mikopo ya vikundi inayotolewa na halmashauri ili kuongeza uwezo wa kumiliki pikipiki zao badala ya kutegemea pikipiki za mikataba zenye masharti magumu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Martin Chung’ong, aliahidi kuwa Balozi wa Arumeru kwa kusaidia kuwaunganisha wananchi wa eneo hilo na fursa mbalimbali za kimataifa.
Chung’ong aliwataka waendesha bodaboda kutekeleza majukumu yao kwa weledi, akisema wanapaswa kutambua nafasi yao katika kuitangaza Tanzania kwa wageni wanaotembelea Arusha.
Aliahidi kuchangia dola za Marekani 200 kwa ajili ya ununuzi wa kompyuta itakayotumiwa katika ofisi hiyo, huku Benki ya NMB nayo ikiahidi kutoa kichapishi (printer) kwa ajili ya kurahisisha shughuli za kiutawala.
Naye Katibu wa Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Arusha, Hakim Msemo, alimpongeza Lugangira kwa kukutana na kundi hilo na kuonesha utayari wa kushughulikia changamoto zao.
Msemo alisema wanatarajia ushirikiano huo utasaidia kuboresha mazingira ya kazi zao na kuimarisha nafasi ya waendesha bodaboda katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Ends..











Post a Comment