LUGANGIRA ATANGAZA VITA UPOTEVU WA MAPATO MERU
...Aanzisha mfumo wa wananchi kuripoti kero moja kwa moja kwake, aonya watumishi wazembe
Aagiza tathmini ya mapato ya masoko, minada, migodi ya kokoto na hoteli
Na Joseph Ngilisho | MERU
MKUU wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, ametangaza hatua za kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru, akionya kuwa hatamkingia kifua mtumishi au mtu yeyote atakayebainika kuchangia upotevu wa fedha za umma.
Aidha, ameandaa utaratibu maalumu utakaowawezesha wananchi kuwasilisha kero na malalamiko yao moja kwa moja kwake, akilenga kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kuhakikisha changamoto za wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Lugangira alitoa kauli hiyo oktoba 16,2026 wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Meru, ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kukutana na makundi mbalimbali ya wadau ili kuhimiza na kuboresha utendaji kazi, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Alisema dhamira yake ni kuhakikisha rasilimali za Serikali zinasimamiwa ipasavyo, mapato yote yanayostahili kukusanywa yanaingia kwenye mifumo rasmi na miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha zilizotumika (value for money).
Katika hatua ya kuimarisha usimamizi wa mapato, Lugangira amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuwasilisha taarifa za makusanyo kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwamo masoko, minada, magulio, migodi ya kokoto, maegesho ya magari na ushuru wa huduma (service levy) kutoka kwa wafanyabiashara na hoteli.
Alisema taarifa hizo zitamwezesha kufanya tathmini ya mwenendo wa mapato, kubaini mianya ya upotevu na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi wa ukusanyaji bila kuwaongezea wananchi na wafanyabiashara tozo zisizostahili.
“Kinachotakiwa kufika kwa Serikali, kifike kwa Serikali. Nataka tushirikiane katika kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato,” alisema.
Lugangira, ambaye ana taaluma katika masuala ya manunuzi, ugavi na teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT), alisema atatumia ujuzi wake kuchunguza mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato ili kubaini mapungufu yanayoweza kusababisha fedha za umma kupotea.
Alisisitiza kuwa hatakubaliana wala kumlinda mtu yeyote atakayebainika kuchangia upotevu wa mapato ya Serikali, akieleza kuwa ukusanyaji wenye ufanisi ni msingi muhimu wa kuimarisha uwezo wa halmashauri kugharamia huduma na miradi ya maendeleo.
WANANCHI KUMFIKIA MOJA KWA MOJA
Katika mkakati mwingine wa kuimarisha uwajibikaji, Lugangira alisema atatoa namba maalumu ya simu kwa wananchi ili waweze kuwasilisha kero na changamoto zao moja kwa moja kwake.
Alisema utaratibu huo utasaidia kubaini malalamiko ambayo yamekuwa yakikwama katika ngazi za chini, licha ya wananchi kuyawasilisha kwa watumishi wenye dhamana ya kuyashughulikia.
Alieleza kuwa mwananchi atakayetumia mfumo huo atatakiwa kutaja jina lake, eneo analotoka, aina ya kero inayomkabili, muda ambao tatizo limekuwepo na hatua alizochukua kabla ya kuwasilisha malalamiko hayo.
“Unapoona mwananchi anachukua simu na kupeleka kero yake nje ya watumishi wanaopaswa kuishughulikia, inaonyesha kuna changamoto,” alisema.
Alionya kuwa hatakubali watumishi kupuuza malalamiko ya wananchi kwa makusudi, akisisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa uadilifu na kwa kuzingatia dhamana aliyopewa.
“Siwezi kukubali Serikali ifanye jitihada za kuwaletea wananchi maendeleo, halafu sisi tuliopata dhamana ya kuwatumikia tushindwe kufanya kazi yetu kwa ufasaha,” alisema.
Lugangira alisema mpango wake wa kukutana na makundi mbalimbali katika wilaya hiyo unalenga kujenga ushirikiano kati ya uongozi, watumishi na wananchi ili kuboresha huduma za umma na kuongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Alisema dhamira yake ni kuifanya Arumeru kuwa wilaya ya mfano na yenye viwango vya kimataifa, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yanahitaji nidhamu ya kazi, usimamizi mzuri wa mapato na uwajibikaji wa kila mtumishi.
Aliongeza kuwa fursa zinazotokana na ukuaji wa Jiji la Arusha, utalii, mikutano ya kimataifa na shughuli nyingine za kiuchumi zinapaswa kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wa Arumeru kupitia mipango madhubuti ya maendeleo na usimamizi bora wa rasilimali za umma.
Ends


Post a Comment