Ad
Breaking🔥

KADOGOSA AMTIMUA KAZI MENEJA TANROADS MZIGO,ADAI HARIDHISHWI NA USIMAMIZI WAKE WA MRADI

KADOGOSA AMUONDOA KAMU WA TANROADS SONGWE

....AAMURU MKANDARASI KUKAMILISHA BARABARA YA TUNDUМА NDANI YA WIKI MBILI

Na Joseph Ngilisho | SONGWE

WAZIRI wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, amemuondoa katika nafasi ya Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe, Mhandisi Fredrick Mande, na kumtaka kurejea makao makuu ya wakala huo, akieleza kutoridhishwa na usimamizi wa ujenzi wa barabara muhimu ya Forodha–OSBP–Tunduma, mpakani mwa Tanzania na Zambia.

Hatua hiyo imekuja baada ya Kadogosa kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa mita 1,675 usiku wa Oktoba 15, 2026, kufuatia maelekezo ya Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, aliyekuwa ameeleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo licha ya Serikali kutoa sehemu kubwa ya fedha zilizohitajika.

Katika hatua nyingine, Kadogosa amempa mkandarasi anayetekeleza mradi huo muda wa wiki mbili kukamilisha kazi zilizobaki, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili kurahisisha shughuli za usafirishaji na biashara katika mpaka wa Tanzania na Zambia.

Waziri huyo amesema atarejea katika eneo la mradi ndani ya siku saba zijazo kukagua hatua zilizofikiwa na kujiridhisha iwapo mkandarasi ametekeleza maagizo yaliyotolewa.

Amesema Serikali haitasita kuchukua hatua kwa viongozi na watendaji wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, hasa katika miradi ya miundombinu inayotumia fedha za umma.

Kadogosa pia amesema taratibu zinaendelea za kumpata meneja mwingine atakayesimamia shughuli za TANROADS Mkoa wa Songwe, kufuatia kuondolewa kwa Mande katika nafasi hiyo.

Barabara hiyo ni muhimu kwa shughuli za forodha, usafirishaji wa mizigo na biashara ya mipakani, hivyo ucheleweshaji wa ujenzi wake unaweza kuathiri ufanisi wa huduma kwa wafanyabiashara na wasafirishaji wanaotumia mpaka wa Tunduma.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post