DC LUGANGIRA AOMBA USHIRIKIANO WA VIONGOZI WA KIMILA KUHARAKISHA MAENDELEO ARUMERU
...Apongeza jamii za Kimaasai na Wameru kwa kulinda amani, umoja na mshikamano
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MKUU wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, amewaomba viongozi wa kimila wa jamii za Kimaasai na Wameru kushirikiana na Serikali katika kuharakisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kuimarisha ustawi wa wananchi wa wilaya hiyo.
Lugangira ametoa ombi hilo wakati wa ziara yake ya kuwatembelea viongozi hao kwa lengo la kujitambulisha, kueleza mipango ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kimila katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema ushirikiano wa viongozi wa kimila ni muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo, kuimarisha umoja wa jamii na kudumisha amani na utulivu katika Wilaya ya Arumeru, inayojumuisha Halmashauri za Arusha na Meru.
Katika ziara hiyo, Lugangira amewapongeza viongozi hao kwa kutambua umuhimu wa amani, umoja na mshikamano, akiwataka kuendeleza juhudi za kulinda tunu hizo ambazo ni msingi wa maendeleo ya jamii.
Aidha, amewahimiza kuendelea kuheshimu, kulinda na kurithisha mila na desturi zinazojenga jamii, huku wakizingatia maadili ya Taifa yanayosisitiza upendo, amani, utulivu na mshikamano.
Kwa upande wao, viongozi hao wa kimila wamemshukuru Lugangira kwa kuwatembelea na kuonyesha unyenyekevu, wakiahidi kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia wananchi wa Arumeru.
Viongozi hao ni Laigwanani Mkuu Isack Ole Kisongo Meijo, Mwenyekiti Mkuu wa Viongozi wa Jamii ya Kimaasai nchini Tanzania; Laigwanani Amani Karaine Lukumay, Katibu Mkuu wa Viongozi wa Jamii ya Wamaasai nchini Tanzania; na Mzee Wilson Mbise, Mshili Mkuu wa Jamii ya Wameru.
Wamesema wataendelea kushirikiana na uongozi wa wilaya hiyo katika kuhimiza wananchi kudumisha amani, upendo na mshikamano kupitia maeneo yao na vikao vya kimila.
Viongozi hao wameeleza utayari wao wa kusimama pamoja na Mkuu huyo wa Wilaya katika kutekeleza majukumu yake, wakisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na viongozi wa kimila ni muhimu katika kufanikisha maendeleo na kuimarisha mahusiano ndani ya jamii.
Aidha, wamemuombea Lugangira baraka za Mwenyezi Mungu, wakimtaka aendelee kupewa hekima, maarifa na busara zitakazomsaidia kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuleta maendeleo kwa wananchi wa Arumeru.
Ends







Post a Comment