DC KARANGA AKERWA NA MAHUDHURIO HAFIFU, ATOA ONYO
Na Joseph Ngilisho | KARATU
Dkt. Karanga ametoa kauli hiyo , Oktoba 1, 2026, wakati wa kikao kilichowakutanisha wawakilishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Bodi ya Maji ya Karatu (KARUWASA), watumiaji wa huduma ya maji pamoja na wananchi.
Amesema ushiriki wa wadau katika vikao vya aina hiyo ni muhimu kwa kuwa ndio sehemu ya kujadili changamoto zinazowakabili wananchi, kusikiliza maoni ya pande mbalimbali na kufikia maamuzi yanayolenga kuboresha huduma na maisha ya wananchi.
Kwa mujibu wa Dkt. Karanga, suala la huduma ya maji, ikiwemo upatikanaji wa maji safi na gharama zake, linahitaji ushirikiano wa wadau wote ili changamoto zilizopo ziweze kupata majibu yanayotekelezeka.
“Ni muhimu wadau tushiriki kikamilifu katika vikao hivi kwa sababu tunapokutana ndipo tunapata nafasi ya kujadili changamoto, kusikilizana na kutafuta suluhisho kwa pamoja,” amesema Dkt. Karanga.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usafi katika Mji wa Karatu, akieleza kuwa uongozi wa wilaya hautasita kuchukua hatua dhidi ya watu wanaokiuka maelekezo na taratibu za usafi wa mazingira.
Amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha mazingira ya mji yanakuwa safi, ikiwemo kufanya operesheni za kubaini watu wanaokaidi maelekezo ya usafi na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Dkt. Karanga pia ameonya dhidi ya vitendo vya kushawishi migomo kwa lengo la kukwamisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo, programu za usafi wa mazingira na miradi inayotekelezwa na Serikali.
Amesema hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo, akisisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi na wadau ni muhimu katika kuhakikisha mipango ya maendeleo inatekelezwa bila vikwazo.
Ametoa wito kwa wadau wote, wakiwemo wananchi, taasisi za Serikali na watumiaji wa huduma, kushiriki kikamilifu katika vikao na michakato ya maamuzi inayohusu huduma muhimu za kijamii, ili changamoto zinazowakabili wananchi zipate ufumbuzi wa pamoja.
Ends

Post a Comment