WAJUMBE 400,NA NCHI 48 KUTUA ARUSHA KONGAMANO LA KODI ARUSHA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Mkutano huo utafanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026, katika Hoteli ya Gran Meliá, huku Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi akitarajiwa kuwa mgeni rasmi na kuufungua rasmi mkutano huo Oktoba 6.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo septemba 30,2026 Mkuu wa Mkoa wa Arusha alisema ujio wa wajumbe hao ni fursa kubwa kwa jiji hilo na Tanzania kwa ujumla, hasa katika kukuza utalii, biashara, huduma na uwekezaji.
Alisema zaidi ya wajumbe 400 watakaofika Arusha wataongeza shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali, ikiwemo hoteli, usafirishaji, migahawa, biashara na huduma zinazohusiana na utalii na mikutano.
“Wajumbe hawa wanapokuja Arusha wanapata nafasi ya kwenda Ngorongoro, Tarangire, Serengeti na kuona Mlima Kilimanjaro. Hii ni fursa kubwa ya kuitangaza Tanzania na vivutio vyetu vya utalii,” alisema.
Alisema mkutano huo haupaswi kuangaliwa kama tukio la siku chache pekee, bali kama fursa ya kujenga mahusiano yatakayoweza kuleta wageni wengine nchini kwa ajili ya utalii, biashara na uwekezaji.
“Leo wamekuja kwa ajili ya mkutano wa kodi, lakini tukiwahudumia vizuri wanaweza kurudi kama wawekezaji, watalii au kwa shughuli nyingine. Tuwape huduma itakayoacha tabasamu na kuonyesha ukarimu na upendo wa Watanzania,” alisema.
Kwa upande wa ajenda, matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa mapato, kodi za kampuni za kimataifa na ukuaji wa uchumi wa kidijitali yatakuwa miongoni mwa maeneo muhimu yatakayojadiliwa katika mkutano huo.
Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mcha Hasani, alisema mkutano huo utatoa fursa kwa nchi wanachama kubadilishana uzoefu na utaalamu kuhusu matumizi ya teknolojia katika kuboresha ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma kwa walipa kodi.
Alisema mabadiliko ya teknolojia yameifanya biashara kuvuka mipaka ya nchi, hivyo mamlaka za kodi zinahitaji mifumo na utaalamu unaoendana na mazingira mapya ya biashara za kimataifa.
“Tutazungumza masuala ya teknolojia ambayo inatumika katika ukusanyaji wa mapato, hasa kwa kampuni za kimataifa. Pia tutabadilishana uzoefu kuhusu namna nchi mbalimbali zinavyotoa huduma kwa walipa kodi,” alisema.
Mcha alisema moja ya maeneo yatakayojadiliwa ni namna bora ya kushughulikia kodi za kampuni zinazofanya shughuli katika nchi zaidi ya moja, ikiwemo kampuni zenye matawi au shughuli za kibiashara katika mataifa tofauti.
Alisema ushirikiano kati ya mamlaka za kodi ni muhimu kutokana na kuongezeka kwa biashara zinazovuka mipaka.
“Tutabadilishana utaalamu na namna bora ya kutoza kodi kwa kampuni ambazo zinafanya biashara katika nchi moja lakini zina matawi katika nchi nyingine,” alisema.
Aidha, alisema uchumi wa kidijitali (Digital Economy) utakuwa sehemu nyingine muhimu ya mjadala kutokana na kuongezeka kwa biashara na huduma zinazofanyika kupitia mitandao.
Alisema teknolojia imeibua aina mpya za biashara ambazo zinaweza kuhudumia wateja katika nchi mbalimbali bila kampuni kuwa na uwepo wa moja kwa moja katika nchi husika, jambo linalozifanya mamlaka za kodi kutafuta mbinu mpya za usimamizi na ukusanyaji wa mapato.
“Pia tutazungumzia masuala ya kodi ya biashara za kimataifa na digital economy. Kuna biashara nyingi zinafanyika katika nyanja ya huduma za mitandao na biashara mtandaoni. Tutabadilishana uzoefu na ujuzi ili tufanye kazi kwa ufanisi zaidi,” alisema.
Mkuu wa Mkoa alisema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika na hali ya usalama jijini Arusha ni ya kuridhisha.
Aliwataka wananchi, wafanyabiashara na watoa huduma kutumia fursa hiyo kuonyesha utamaduni wa Watanzania wa ukarimu na kuhakikisha wageni wanapata huduma bora.
Alisema huduma nzuri kwa wajumbe hao inaweza kuwa sehemu ya kuitangaza Arusha na Tanzania kwa ujumla, huku wageni hao wakiwa mabalozi wa vivutio na fursa za biashara na uwekezaji watakazoziona nchini.
Pia aliipongeza TRA kwa kuaminiwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo unaoshirikisha nchi 48 za Jumuiya ya Madola, akisema tukio hilo linaipa Tanzania nafasi ya kushiriki katika mijadala ya kimataifa kuhusu mustakabali wa mifumo ya kodi.
Mkutano huo unabeba kaulimbiu: “Matumizi ya Teknolojia katika Kuboresha Ufanisi wa Ukusanyaji wa Mapato.”
Ends





Post a Comment