Breaking🔥

SERIKALI YAMEKEZA MIUNDO MBINU KUKUZA MICHEZO,TFF YALETA SKAUTI AWESO CUP KUIBUA VIPAJI0

MWANAFA: TFF YALETA SKAUTI AWESO CUP KUIBUA VIPAJI

Na Hadija Bagasha, Tanga

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’, amesema Serikali itahakikisha vipaji vinavyopatikana katika michuano ya AWESO CUP 2026 vinatambuliwa na kuendelezwa, huku akiahidi kupeleka skauti wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika mashindano hayo.

MwanaFA amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha vipaji vya vijana havipotei kutokana na kukosa fursa ya kutambuliwa, akieleza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kutumia vipaji vyao kujenga maisha na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Naibu Waziri huyo ameyasema hayo wakati akizindua rasmi michuano ya mpira wa miguu ya AWESO CUP 2026 katika Uwanja wa Sakura, Wilaya ya Pangani, Mkoa wa Tanga.

Amesema mashindano hayo yanayoshirikisha jumla ya timu 80 kutoka ndani ya Jimbo la Pangani ni fursa kubwa ya kuibua vipaji, huku akimhakikishia Mbunge wa Pangani ambaye pia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kuwa Wizara yake itashirikiana na TFF kufuatilia vipaji vitakavyojitokeza.

“Mashindano haya kwa sababu yana timu 80 ni marefu. Nikuhakikishie Mheshimiwa Aweso kwamba hata hapa skauti wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania watafika ili kugundua vipaji na kama vinajitosheleza tuone namna bora ya kuviendeleza,” amesema MwanaFA.

Amesema uwepo wa timu nyingi katika michuano hiyo unaonyesha mwitikio mkubwa wa vijana wa Pangani katika michezo na kwamba ni wajibu wa Serikali na wadau kutumia fursa hiyo kutafuta na kukuza vipaji.

“Nikiwa kama Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, skauti watafika hapa tuone namna tunaweza kuwapa nafasi na fursa ya kuwakutanisha na riziki zao kutokana na vipaji alivyowajaalia Mwenyezi Mungu,” amesema.

Serikali yaongeza uwekezaji

MwanaFA amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka msukumo katika maendeleo ya sekta ya michezo kwa kuwekeza katika miundombinu pamoja na kuweka mazingira bora ya kukuza vipaji vya vijana.

Amesema uwekezaji huo unahusisha ujenzi na ukarabati wa viwanja mbalimbali nchini, akitaja Uwanja wa Benjamin Mkapa na miundombinu ya michezo katika maeneo mengine, pamoja na ujenzi wa viwanja 15 vya mazoezi.

Kwa mujibu wa MwanaFA, uwekezaji huo unaenda sambamba na mkakati wa Serikali wa kuhakikisha vipaji vinagunduliwa, kulelewa na kutunzwa kuanzia ngazi za chini hadi kufikia hatua ya vijana hao kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Ametoa mfano wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, akisema mafanikio na ushindani wake katika mashindano ya kimataifa yanaonyesha umuhimu wa kuwekeza katika malezi ya vipaji kuanzia ngazi za chini.

Ampongeza Aweso

MwanaFA amempongeza Waziri wa Maji na Mbunge wa Pangani, Jumaa Aweso, kwa kuandaa AWESO CUP 2026, akisema michuano hiyo imefungua fursa kwa vijana kushiriki michezo, kuonyesha uwezo wao na kutambuliwa na wadau wa sekta hiyo.

Amesema mbali na burudani, mashindano hayo yana nafasi ya kuchangia maendeleo ya vijana kwa kuwaunganisha na fursa zinazoweza kuibuka kupitia vipaji vyao.

“Mashindano haya yanatoa picha kubwa ya kivutio na yamekuja wakati sahihi katika kujibu mahitaji ya wananchi na kuibua vipaji vya vijana mbalimbali kupitia mashindano haya,” amesema.



Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa michezo kuhakikisha mashindano yanayoandaliwa katika ngazi za chini yanakuwa sehemu ya mfumo mpana wa kitaifa wa kutafuta, kukuza na kuendeleza vipaji.

Uzinduzi wa AWESO CUP 2026 ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Msemaji wa Timu za Taifa na Diwani wa Kata ya Kariakoo, Haji Manara, pamoja na viongozi wa Serikali na wadau wa michezo.

Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea kutoa burudani kwa wakazi wa Pangani huku ikitoa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao na kwa wafanyabiashara kunufaika na shughuli za kiuchumi zinazozunguka mashindano hayo.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post