Ad
Breaking🔥

DIRA 2050 SILLO ATAKA MATOKEO YAONEKANE KWA WANANCHI

Na Joseph Ngilisho-Arusha

NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daniel Baran Sillo, amesema mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hayapaswi kupimwa kwa idadi ya nyaraka, mikutano au shughuli zilizotekelezwa, bali kwa mabadiliko yanayoonekana katika maisha ya Watanzania.


Sillo alisema hayo leo Septemba 23,2026 wakati akifungua Kongamano la Tano la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza, linalofanyika kwa siku tano kuanzia Septemba 22 hadi 26, katika hoteli ya Ngurdoto likishirikisha wadau zaidi ya 1,500 kutoka ndani na nje ya nchi.

Alisema kongamano hilo linapaswa kuwa chachu ya kuimarisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhakikisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini inaimarishwa na kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia Serikali kufanya maamuzi kwa wakati.

“Ni imani yangu kuwa kongamano hili litaleta hamasa na chachu ya kuimarisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Tunatarajia kuona mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na tathmini ikiimarishwa ili kuhakikisha utekelezaji wa Dira hiyo unapimika, unafuatiliwa kwa uwazi na matokeo yake yanaonekana kwa umma,” alisema.

Alisema Tanzania imeingia katika kipindi cha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kutoa mwelekeo wa taifa hadi mwaka huo, lakini bila mfumo madhubuti wa kupima maendeleo, Dira hiyo inaweza kubaki kuwa azma nzuri iliyoandikwa kwenye nyaraka.

“Ufuatiliaji na tathmini una nafasi ya kipekee katika safari hii.

 Tunahitaji mfumo unaoweza kutuambia hali halisi kila wakati na kwa wakati muafaka,” alisema.

Alisema Dira 2050 haitapimwa kwa idadi ya nyaraka zilizoandaliwa, mikutano iliyofanyika au shughuli zilizotekelezwa pekee, bali kwa kuangalia mabadiliko katika maisha ya wananchi.

Alisema maeneo yatakayotumika kupima mabadiliko hayo ni pamoja na ubora wa elimu, huduma za afya, ajira na tija yake, kipato cha Watanzania, ubora wa miundombinu, upatikanaji wa huduma za msingi, mazingira pamoja na ushiriki wa vijana na wanawake katika maendeleo.

Alisema Tanzania inahitaji uongozi unaopima matokeo, taasisi zinazojifunza, mifumo inayotoa taarifa sahihi na wananchi wanaoshirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Alisema misingi hiyo ndiyo itakayosaidia kujenga Serikali inayowajibika, inayosikiliza wananchi, inayojifunza na kutekeleza mipango kwa kuzingatia matokeo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu–Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dk Jim Yonazi, alisema ofisi yake itaendelea kuratibu juhudi za kuimarisha ufuatiliaji, tathmini na kujifunza kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha mfumo huo unasaidia utekelezaji wa Dira 2050, unaimarisha uwajibikaji na kuwawezesha viongozi kufanya maamuzi kwa wakati na kuboresha huduma kwa wananchi.

Dk Yonazi alisema kaulimbiu ya mwaka huu, “Kutoka Ushahidi Kwenda Vitendo: Kuimarisha Tathmini Inayomweka Binadamu Katikati kwa Maendeleo Endelevu,” imechaguliwa kutokana na umuhimu wa kuhakikisha ushahidi unaopatikana unatumika katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Alisema utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulianza Julai 1, 2026, hivyo Serikali sasa ipo katika awamu ya utekelezaji na si kupanga pekee.

“Hii ni awamu ya utekelezaji na si ya kupanga. Serikali sasa haihitaji taarifa inayoeleza kilichotumika au kilichojengwa pekee; inahitaji ushahidi unaoonyesha kama maisha ya watu yamebadilika, kwa nani, kwa gharama gani na kwa muda gani mabadiliko hayo yatadumu,” alisema.

Alisema kuna hatari ufuatiliaji na tathmini ukageuka kuwa zoezi la kujaza fomu, kutengeneza dashibodi na kuwasilisha ripoti zinazopendeza bila kuonyesha hali halisi ya wananchi.

Alisema msisitizo wa mwaka huu ni kumweka mwananchi katikati ya utekelezaji wa afua na miradi mbalimbali, si kumtazama kama chanzo cha takwimu pekee.

“Mwananchi anapaswa kuwa kitovu cha matunda yoyote ya utekelezaji wa miradi, si kama chanzo cha takwimu, bali kama mshirika anayeshiriki kueleza mafanikio yanapimwaje na kuthibitisha kama hitimisho letu linaakisi hali halisi ya maisha yake,” alisema.

Kongamano hilo linawakutanisha wadau wa ufuatiliaji, tathmini na kujifunza kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa lengo la kujadili namna ushahidi unavyoweza kutumika katika kufanya maamuzi, kuboresha utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kuimarisha uwajibikaji.


Ends


Post a Comment

Previous Post Next Post