TRA YAWEKA MKAKATI WA KUKUSANYA SH TRILIONI 41.4, YALENGA KUBORESHA HUDUMA ZA KODI
Na Joseph Ngilisho | Arusha
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka mikakati mipya ya kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kwa lengo la kufikia makusanyo ya Sh trilioni 41.4 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuongeza mapato ya ndani, kuimarisha mazingira ya biashara na kuhakikisha walipakodi wanapata huduma bora za kodi.
Akizungumza wakati wa kikao cha viongozi wa TRA kilicholenga kupitia utekelezaji wa mipango ya mwaka uliopita na kuweka mikakati ya mwaka mpya wa fedha, Kamishna Mkuu wa TRA amesema mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha lengo hilo linafikiwa kupitia maboresho mbalimbali ya kiutendaji.
Alisema mikakati iliyowekwa inalenga kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari, kupanua wigo wa walipakodi, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato pamoja na kurahisisha huduma kwa wafanyabiashara na wananchi.
“TRA itaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kushirikiana na walipakodi, kuhakikisha huduma za kodi zinakuwa rahisi, za haraka na zenye ufanisi ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa,” alisema.
Aliongeza kuwa mamlaka hiyo imefanyia kazi maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kilele cha Tuzo za Rais za Walipakodi pamoja na maelekezo ya Rais wa Zanzibar yaliyotolewa katika kikao cha Baraza la Mapinduzi, kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa na matokeo chanya.
Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu, mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita yamejenga msingi imara wa kufikia malengo makubwa ya ukusanyaji wa mapato, huku akiwapongeza watumishi wa TRA kwa juhudi zao zilizowezesha mamlaka hiyo kuvunja rekodi mbalimbali za makusanyo.
Amesema watumishi na ofisi zilizofanya vizuri zaidi zitaendelea kutambuliwa na kupewa tuzo kama njia ya kuhamasisha uwajibikaji na kuongeza ari ya utendaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria wa TRA, Elisha Shigela, kwa niaba ya Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, alisema ushirikiano, uzingatiaji wa maadili na utekelezaji wa maelekezo ya viongozi ni mambo muhimu katika kufikia malengo ya taasisi hiyo.
Aliwataka watumishi wa TRA kuendelea kufanya kazi kwa mshikamano na kuzingatia misingi ya taasisi ikiwemo weledi, uwajibikaji, uadilifu na uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Alisema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi kilichopita yametokana na kujituma kwa watumishi wote, hivyo ari hiyo inapaswa kuendelezwa ili kuhakikisha malengo ya mwaka huu wa fedha yanafikiwa.
“Nawakumbusha watumishi kuendelea kuzingatia misingi ya taasisi ikiwemo weledi, uwajibikaji, uadilifu na uzalendo, kwa kuwa hayo ndiyo msingi wa utoaji wa huduma bora na mafanikio ya TRA,” alisema Shigela.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Uledi Mussa, alisema mafanikio ya ukusanyaji wa mapato yanayotokana na mamlaka hiyo si ya bahati, bali yamechangiwa na umoja, mshikamano, nidhamu na uwajibikaji wa viongozi na watumishi.
Alisema mazingira mazuri ya kazi yenye ushirikiano huongeza ufanisi na kuwafanya watumishi kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kujituma zaidi.
“Mafanikio haya yametokana na ushirikiano wa pamoja kati ya viongozi na watumishi. Umoja huu umeendelea kuwa chachu ya kuimarika kwa makusanyo ya kodi,” alisema.
Aidha, Uledi alisema TRA imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika kutokana na juhudi zake za kutoa elimu ya kodi kwa wananchi na walipakodi kupitia njia mbalimbali.
Alitolea mfano nchi ya Ghana ambayo imekuwa ikijifunza kutoka Tanzania kuhusu mbinu za kuongeza uelewa wa walipakodi na kuimarisha ulipaji wa kodi kwa hiari.
Alisema TRA itaendelea kuimarisha mahusiano na walipakodi, kuboresha huduma na kutumia mifumo ya kisasa ili kuongeza mapato ya ndani na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Ends

Post a Comment