TANZANIA KUANDAA MKUTANO WA KIMATAIFA WA COP12 WA MKATABA WA NAIROBI OKTOBA
Na Hadija Bagasha |Tanga
SERIKALI imetangaza rasmi kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), hatua inayotarajiwa kuimarisha nafasi ya nchi katika uongozi wa uhifadhi wa mazingira ya bahari, kukuza uchumi wa buluu na kufungua fursa mpya za uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa.
Mkutano huo utafanyika kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ukitarajiwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya 600 kutoka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi pamoja na taasisi mbalimbali za kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, amesema uenyeji wa mkutano huo unaonesha imani kubwa ambayo jumuiya ya kimataifa imeendelea kuiweka Tanzania katika juhudi za kuhifadhi mazingira ya bahari na ukanda wa pwani.
Amesema mkutano huo utawakutanisha viongozi wa serikali, wataalamu na wadau mbalimbali kujadili utekelezaji wa Mkataba wa Nairobi, usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari, mapambano dhidi ya uchafuzi wa mazingira, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na mikakati ya kukuza uchumi wa buluu.
"Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa COP12, hatua inayodhihirisha nafasi yake katika uongozi wa uhifadhi wa mazingira ya Bahari ya Hindi na kufungua fursa mpya za uwekezaji, ushirikiano wa kimataifa na maendeleo ya uchumi wa buluu," amesema Kwagilwa.
Ameeleza kuwa mkutano huo pia utajadili mikakati ya kurejesha mifumo ikolojia ya bahari, ikiwemo mikoko, miamba ya matumbawe na nyasi bahari, sambamba na kuimarisha utekelezaji wa mikataba ya kimataifa inayolenga kulinda bioanuai za baharini.
Kwa mujibu wa Kwagilwa, Serikali tayari imeunda kamati mbalimbali za kitaifa kwa kushirikiana na wizara, taasisi za umma, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha maandalizi yote yanakamilika kwa wakati na Tanzania inaandaa mkutano wa viwango vya kimataifa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda, amesema maandalizi ya mkutano huo yameanza rasmi yakilenga kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na fursa za kidiplomasia, kiuchumi na kitaalamu zitakazotokana na uenyeji huo.
Amesema washiriki kati ya 500 na 600 kutoka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi pamoja na taasisi za kimataifa wanatarajiwa kushiriki, jambo litakaloipa Tanzania fursa ya kuonesha uwezo wake wa kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa na kuvutia wawekezaji.
Luvanda amesema COP12 pia itakuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za kukabiliana na changamoto zinazoikabili bahari, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuweka mikakati ya matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Buriani, amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zimeanza kuathiri kwa kiwango kikubwa sekta ya uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji, hali inayotishia uchumi wa wananchi wanaotegemea bahari kwa maisha yao.
Amesema utafiti uliofanyika mkoani Tanga kati ya mwaka 2021 na 2025 umeonesha kuwa joto la bahari limeongezeka kutoka nyuzi joto 25.6 mwaka 2021 hadi nyuzi joto 28.39 mwaka 2024, hali inayobadili mifumo ya ikolojia na kupunguza uzalishaji wa sekta ya uvuvi.
Aidha, amesema siku ambazo wavuvi wanaweza kwenda baharini zimepungua kutoka siku 221 mwaka 2021 hadi siku 170 kutokana na kuongezeka kwa upepo mkali na hatari za usalama baharini, huku mavuno ya samaki yakishuka kwa wastani wa asilimia 25 hadi 30.
Kauli hizo zinaakisi umuhimu wa mkutano wa COP12 kwa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo pamoja na kujadili sera na mikakati ya uhifadhi wa mazingira ya bahari, mkutano huo unatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha uchumi wa buluu, kuvutia uwekezaji, kuongeza ushirikiano wa kimataifa na kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ends





Post a Comment