SERIKALI KUJENGA GATI JIPYA BANDARI YA TANGA BAADA YA MAPATO KUPAA MARA TISA

 SERIKALI KUJENGA GATI JIPYA BANDARI YA TANGA BAADA YA MAPATO KUPAA MARA TISA

Na Hadija Bagasha-Tanga

Serikali imetangaza ujenzi wa gati jipya lenye urefu wa mita 300 katika Bandari ya Tanga kufuatia ongezeko kubwa la shughuli za biashara na usafirishaji wa mizigo, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa bandari hiyo ambayo sasa imeanza kuzidiwa na mahitaji ya huduma.

Uamuzi huo unakuja baada ya Bandari ya Tanga kushuhudia mafanikio makubwa kufuatia maboresho yaliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ambapo mapato yanayokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka kutoka Sh bilioni 31 hadi Sh bilioni 298.7 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, huku kiwango cha mizigo inayopitia bandarini kikipanda kutoka tani 750,000 hadi tani milioni 2.7.

Akizungumza leo alipokagua maendeleo ya miundombinu ya Bandari ya Tanga, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alisema Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa utakaoongeza uwezo wa bandari kuhudumia meli nyingi zaidi na kukidhi ongezeko la biashara ya ndani na nje ya nchi.

Alisema ujenzi wa gati hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuendelea kuimarisha sekta ya usafirishaji na uchumi wa Taifa kupitia uwekezaji katika miundombinu ya kisasa.

"Kuna jitihada kubwa zinazofanyika kuendeleza mradi wa upanuzi wa Bandari ya Tanga ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya huduma. Mradi huu unalenga kurahisisha usafirishaji na kuimarisha nafasi ya Tanga kama kitovu muhimu cha biashara na uchumi nchini," alisema Waziri Omar.

Alibainisha kuwa pamoja na upanuzi wa bandari, Serikali itaendelea kuwekeza katika reli, viwanja vya ndege na mtandao wa barabara ili kuhakikisha mifumo yote ya usafirishaji inaunganishwa na kuongeza ushindani wa uchumi wa Tanzania.

Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega, alisema maboresho yaliyofanyika bandarini yameibadilisha Tanga kuwa moja ya bandari zinazokua kwa kasi nchini, jambo lililosababisha kuongezeka kwa idadi ya meli na shehena ya mizigo inayohudumiwa.

Alisema ongezeko hilo limeifanya bandari hiyo kufikia ukomo wa uwezo wake wa sasa, hivyo Serikali imepanga kuanza ujenzi wa gati jipya la mita 300 katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Mbega alisema mbali na gati hilo, Serikali pia imepanga kujenga gati maalumu la mafuta pamoja na gati la kuhudumia meli za makontena, miradi ambayo itaiwezesha Bandari ya Tanga kushindana kwa kiwango kikubwa zaidi na bandari nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Burian, alisema Mkoa umeanza maandalizi ya kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kuhifadhi mafuta (Oil Terminals), hatua itakayoongeza usalama wa upatikanaji wa nishati na kuvutia uwekezaji wa viwanda.

Alisema maendeleo ya Bandari ya Tanga yataufanya mkoa huo kuwa kitovu kikubwa cha biashara, usafirishaji na huduma za nishati kwa Kaskazini mwa Tanzania na nchi jirani.

Katika ziara hiyo, Waziri Omar pia alitangaza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi mingine ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa barabara ya Tanga–Pangani yenye urefu wa kilomita 50 pamoja na barabara ya Handeni–Singida ili kuunganisha Bandari ya Tanga na maeneo makubwa ya uzalishaji, kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ufanisi wa biashara.

Aidha, aliupongeza uongozi wa Mkoa wa Tanga na TPA kwa kusimamia kwa mafanikio mradi wa maboresho ya Bandari ya Tanga uliogharimu Sh bilioni 429.1, akieleza kuwa ndani ya takribani mwaka mmoja tangu kukamilika kwake, Serikali tayari imekusanya zaidi ya Sh bilioni 436 kutokana na shughuli za bandari hiyo.

Alisema mafanikio hayo yanaonyesha kuwa uwekezaji wa Serikali umeanza kutoa matokeo chanya kwa uchumi wa Taifa na kuongeza mchango wa Bandari ya Tanga katika biashara ya kikanda na kimataifa.

Waziri Omar alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya Bandari ya Tanga ili kuifanya kuwa lango kuu la biashara kwa ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania na nchi jirani, sambamba na kuongeza mapato ya Serikali, ajira na ukuaji wa uchumi.







Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post