RUNGWE AVUNJA UKIMYA, AANIKA SABABU ZA KUMTIMUA KATIBU MKUU WA CHAUMMA
Na Arushadigital | Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Taifa, Mzee Hashim Rungwe Spunda, amevunja ukimya na kuweka wazi sababu zilizomfanya kumvua madaraka aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu Juma, akisema hatua hiyo imelenga kurejesha nidhamu, kulinda Katiba ya chama na kuimarisha misingi ya uongozi bora.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 1, 2026, katika Makao Makuu ya CHAUMMA jijini Dar es Salaam, Rungwe alisema uamuzi huo ulianza kutekelezwa rasmi Juni 30, 2026, baada ya kupitishwa na vikao halali vya chama.
Alisema hatua hiyo haikutokana na tofauti za kisiasa bali ni matokeo ya ukiukwaji wa taratibu za uongozi, ambapo alimtuhumu aliyekuwa Katibu Mkuu kwa kubadili maamuzi yaliyokuwa yamepitishwa na vikao vya chama na kuyabadilisha kwa maslahi binafsi.
"Kiongozi yeyote ndani ya chama anatakiwa kuheshimu Katiba, kanuni na maamuzi ya vikao halali. Haiwezekani mtu mmoja kubadili maamuzi ya chama kwa matakwa yake mwenyewe," alisema Rungwe.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, mwenendo huo uliendelea kwa muda na kusababisha mkanganyiko mkubwa katika utendaji wa chama, hali iliyotishia mshikamano wa viongozi na utekelezaji wa maamuzi muhimu ya kisiasa na kiutawala.
Rungwe alieleza kuwa Halmashauri Kuu ya Taifa, kwa ridhaa ya Sekretarieti ya chama iliyokutana jana, iliridhia hatua ya kumwondoa Katibu Mkuu huyo, akisisitiza kuwa uamuzi huo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uwajibikaji na kurejesha heshima ya taasisi za chama.
Alisisitiza kuwa CHAUMMA kitaendelea kusimamia misingi ya uwazi, uwajibikaji na utawala wa sheria bila kumvumilia kiongozi yeyote atakayekiuka Katiba na kanuni za chama, bila kujali nafasi yake.
Hatua hiyo inatajwa kuwa mwanzo wa mageuzi mapya ndani ya CHAUMMA, huku uongozi wa chama ukiahidi kuendelea kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wote watakaokiuka maadili na taratibu zilizowekwa kwa maslahi ya chama na wanachama wake.
Ends...

Post a Comment