RAJABU: CCM IJIPIME KWA UTEKELEZAJI WA ILANI, SI MANENO
Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Mlezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Rajabu Abdulrahman, amewataka viongozi wa chama na serikali kujipima kwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi badala ya kutegemea kauli za kisiasa, akisisitiza kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi ujao utategemea kiwango cha kutimiza ahadi walizozitoa kwa wananchi.
Rajabu alitoa kauli hiyo leo Julai 4,2026 jijini Arusha wakati akifungua kikao maalumu cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Arusha cha tathmini ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, katika kikao cha halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Arusha.
Alisema chama hakipaswi kusubiri kipindi cha uchaguzi ndipo kianze kueleza mafanikio yake, bali kinapaswa kufanya tathmini endelevu ya utekelezaji wa kila ahadi ili kubaini mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji maboresho.
"Ikiwa tumewaahidi wananchi kutekeleza malengo fulani ndani ya miaka mitano, lazima kila mwaka tujipime kuona tumefikia kiwango gani. Tukiona hatuendi kwa kasi iliyokusudiwa, tuchukue hatua mapema badala ya kusubiri mwisho wa kipindi," alisema Rajabu.
Alisisitiza kuwa vikao vya chama kuanzia wilayani hadi mkoani vinapaswa kuwa sehemu ya kutathmini utekelezaji wa ilani na kutafuta suluhisho la changamoto zinazojitokeza, badala ya kubaki kuwa vikao vya kawaida vya taarifa.
Rajabu alisema imani ya wananchi kwa CCM na serikali yake itaendelea kuimarika endapo viongozi wataonyesha uwajibikaji kwa kutekeleza ahadi walizopewa dhamana ya kuzisimamia.
"Wananchi wataendelea kutuamini wakiona yale tuliyowaahidi yanatekelezwa kwa vitendo. Tusikubali imani hiyo ishuke kwa sababu ya uzembe katika utekelezaji wa majukumu yetu," alisema.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Arusha, Ramsey Saipulan, alisema chama hakitakuwa na muhali kwa kiongozi yeyote wa serikali atakayeshindwa kutekeleza Ilani ya CCM, akisisitiza kuwa viongozi wote watawajibishwa kwa maslahi ya wananchi.
Alisema tathmini ya utekelezaji wa ilani katika wilaya zote saba za Mkoa wa Arusha imeonesha mafanikio makubwa, lakini pia imebaini maeneo yanayohitaji usimamizi na ufuatiliaji wa karibu.
"Hatutakuwa na soni wala hofu kwa kiongozi yeyote ambaye uzembe wake utakwamisha utekelezaji wa Ilani ya CCM. Serikali ipo kutekeleza ilani, na sisi kama chama tuna wajibu wa kuhakikisha ahadi zote kwa wananchi zinatekelezwa kwa wakati na kwa ubora," alisema.
Saipulan alisema CCM itaongeza kasi ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kwa kufanya tathmini za mara kwa mara, kupokea taarifa za utekelezaji kila baada ya miezi sita na kutembelea miradi ili kujiridhisha kuhusu matumizi ya fedha za umma pamoja na ushirikishwaji wa wananchi.
"Tutahoji, tutafuatilia na tutawawajibisha wote watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao. Wananchi waliiamini CCM kwa sababu ya ilani yake, hivyo hatutaruhusu ahadi hizo zibaki kwenye karatasi," alisema.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya chama na serikali unapaswa kupimwa kwa matokeo yanayogusa maisha ya wananchi kupitia huduma bora za maji, afya, elimu, barabara na miradi mingine ya maendeleo.
Saipulan alisema wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Arusha pia wamempongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua kubwa za utekelezaji wa Ilani ya CCM na kueleza kuwa tathmini hiyo imekipa chama picha halisi ya utekelezaji wake katika mkoa huo.
"Hatutasubiri mwaka wa uchaguzi ndipo tuanze kuulizana maswali. Kazi yetu ni kuhakikisha kila ahadi iliyotolewa kwa wananchi inatekelezwa kwa wakati, kwa sababu mwisho wa siku ni CCM ndiyo itakayoulizwa na wananchi kuhusu utekelezaji wa ilani yake," alisema.
Ends..


















Post a Comment