MWANG'ONDA: RAIS SAMIA ANATIMIZA AHADI YA KUMTUA MAMA NDOO KICHWANI

MWANG'ONDA: RAIS SAMIA ANATIMIZA AHADI YA KUMTUA MAMA NDOO KICHWANI

Na Joseph Ngilisho, Arusha

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang'onda, amezindua mradi wa ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita 50,000 katika eneo la Kimindorosi, Kata ya Olasiti, Wilaya ya Arusha, akisema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha upatikanaji wa huduma za maji na "kumtua mama ndoo kichwani."

Mradi huo uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) ulizinduliwa leo Julai 9, 2026, ikiwa ni sehemu ya miradi inayotembelewa na Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Arusha.

Akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa AUWSA, Kazimili Reuben Kanyanza, alisema mradi umejengwa na mafundi wa mamlaka hiyo kwa gharama ya jumla ya shilingi milioni 95.8, ambapo shilingi milioni 2.5 zimetolewa na wananchi kupitia nguvu na michango yao, huku Serikali Kuu ikitoa shilingi milioni 93.3.

Alisema utekelezaji wa mradi huo umeongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi kwa wakazi wa Kimindorosi na maeneo ya jirani, hivyo kupunguza adha ya wananchi, hususan wanawake na watoto, waliokuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo, Mwang'onda aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maji nchini, akisema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya dhati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma muhimu karibu na makazi yake.

Alisema miradi ya maji ni miongoni mwa miradi yenye matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi kwa kuwa inaboresha afya, mazingira na shughuli za kiuchumi.

"Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wananchi wanapata maji karibu na maeneo yao. Leo kina mama wa Kimindorosi wanashuhudia kwa vitendo kutokomeza adha ya kubeba ndoo kichwani na kutembea umbali mrefu kutafuta maji," alisema Mwang'onda.

Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan sekta ya maji, jambo linalodhihirisha kuwa ahadi zinazotolewa kwa wananchi zinageuzwa kuwa vitendo.

Katika hatua nyingine, Mwang'onda alisema Mwenge wa Uhuru ukiwa Wilaya ya Arusha utakimbizwa umbali wa kilomita 89.2 na kutembelea, kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kukagua jumla ya miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.9.

Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 inasema: "Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuijenga."




Endss

Post a Comment

Previous Post Next Post