MVUTANO WAIBUKA TANGA BAADA YA MABASI KUHAMISHIWA STENDI YA KANGE
Na Hadija Bagasha, Tanga
Mvutano umeibuka mkoani Tanga kufuatia uamuzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga kuanza kutekeleza rasmi agizo la kuhamishia mabasi yote ya safari za mikoani katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange, huku wamiliki wa mabasi, wasafiri na wadau wa usafirishaji wakilalamikia utekelezaji wa hatua hiyo.
Uamuzi huo umeondoa utaratibu wa mabasi kupakia na kushusha abiria katikati ya jiji na katika ofisi za kampuni mbalimbali za usafirishaji, kwa lengo la kuhakikisha Stendi ya Kange inatumika kikamilifu kwa mujibu wa sheria na kuboresha huduma za usafiri.
Hata hivyo, Umoja wa Wasafirishaji Mkoa wa Tanga (TABOA) umesema haupingi matumizi ya stendi hiyo, bali unalalamikia uamuzi wa kuanza utekelezaji kabla ya kukamilika kwa huduma muhimu walizokubaliana na Halmashauri.
Makamu Mwenyekiti wa TABOA Mkoa wa Tanga, Albert Peter, alisema viongozi wa jiji waliwakutanisha mapema mwezi Juni na kuwaeleza mpango wa kuhamishia mabasi yote Kange, ambapo walikubaliana kwanza kuboresha miundombinu na huduma muhimu.
Alitaja baadhi ya huduma walizoomba kuwa ni viti vya kukaa abiria, kituo cha polisi, zahanati, duka la dawa, maeneo ya chakula pamoja na maegesho ya daladala ili kituo hicho kiweze kutoa huduma bora kwa wasafiri.
"Hatupingi Stendi ya Kange. Tunafahamu imejengwa kwa gharama kubwa na lazima itumike, lakini tulitaka kwanza mazingira yawe rafiki kwa wasafiri. Leo tumelazimishwa kuhamia wakati huduma muhimu bado hazijakamilika," alisema Albert.
Aliongeza kuwa TABOA ilifanya ukaguzi wa pamoja na viongozi wa Jiji na kubaini mapungufu yaliyopaswa kurekebishwa kabla ya mabasi kuanza kutumia kituo hicho.
Kwa mujibu wa Albert, kutokuwepo kwa huduma za afya ni moja ya changamoto kubwa kwani endapo msafiri atapata dharura atalazimika kusafirishwa umbali wa takribani kilomita tisa kufuata matibabu.
Pia TABOA imependekeza mabasi yaruhusiwe kuendelea kupakia abiria kwenye vituo vyao vya zamani kwa muda wakati maboresho yakikamilishwa, kabla ya kupitia Stendi ya Kange kwa ajili ya kulipa ushuru wa Sh5,000 kwa siku kama ilivyoelekezwa.
Wakati huo huo, baadhi ya wasafiri wameeleza kutoridhishwa na namna zoezi hilo lilivyotekelezwa, wakidai hawakupewa taarifa za kutosha kuhusu mabadiliko hayo.
Mmoja wa wasafiri, Zunda Rashid Hassan, alisema wengi walifika mjini kama ilivyo kawaida lakini wakakuta mabasi yanazuiwa kuondoka huku wakikosa taarifa za mahali pa kuanzia safari.
"Hatukupewa taarifa mapema. Tumefika tangu asubuhi lakini hatujui tunaondoka saa ngapi. Wengine tuna safari za dharura za kwenda kuwaona wagonjwa, lakini tumekwama," alisema.
Naye Esther Ngao alisema utaratibu huo unaongeza gharama kwa wananchi kwa kuwa sasa wanalazimika kutumia usafiri wa ziada kufika Stendi ya Kange kabla ya kuanza safari zao.
Katika utekelezaji wa agizo hilo, mabasi ya kampuni za Tashriff, Ratco, Abood na Royal Line yalizuiwa katika Stendi ya Kange baada ya kudaiwa kupakia abiria mjini kinyume cha maelekezo ya Halmashauri ya Jiji.
Mwanasheria wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Sebastian Banda, alisema kila basi lililokiuka utaratibu huo lilitozwa faini ya Sh250,000.
"Tumewapatia control number za malipo. Wakilipa faini wataendelea na safari zao. Hatua hii inalenga kuhakikisha sheria za matumizi ya vituo vikuu vya mabasi zinazingatiwa," alisema Banda.
Akizungumzia malalamiko hayo, Meya wa Jiji la Tanga, Mustapha Muhina maarufu Seleboss, alisema uamuzi wa kuhamishia mabasi Kange haujakurupushwa bali unatekeleza sheria na maelekezo ya Serikali.
Alisema awali utekelezaji ulisitishwa kufuatia ushauri wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, ili kutoa nafasi ya kuboresha mazingira ya stendi hiyo.
Muhina alisema baadaye Halmashauri ilipokea barua kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI iliyoelekeza matumizi ya vituo vikuu vya mabasi kusimamiwa kwa mujibu wa sheria.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji, safari zote za mabasi ya mikoani zinapaswa kuanzia katika kituo kikuu cha mabasi, hivyo mabasi yanayoelekea Dar es Salaam, Arusha na mikoa mingine yanatakiwa kuanzia Stendi ya Kange.
Hata hivyo, alisema ili kupunguza usumbufu kwa wananchi, Halmashauri imeweka utaratibu wa mpito ambapo mabasi yanayoondoka alfajiri yataendelea kupakia abiria kwenye ofisi zao zilizopo mjini, huku yale yanayoanza safari kuanzia saa moja asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni yakitakiwa kuanzia safari katika Stendi ya Kange.
Alisisitiza kuwa Jiji litaendelea kuboresha huduma za usafiri wa daladala na miundombinu ya Stendi ya Kange ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama, bora na za uhakika.
Ends



Post a Comment