MKUDE AZINDUA JUKWAA LA VIJANA ARUSHA, AWATAKA KUNUFAIKA NA FURSA ZA KIUCHUMI KUELEKEA MAPOKEZI YA MWENGE WA UHURU

MKUDE AZINDUA JUKWAA LA VIJANA ARUSHA, AWATAKA KUNUFAIKA NA FURSA ZA KIUCHUMI KUELEKEA MAPOKEZI YA MWENGE WA UHURU

Na Joseph Ngilisho| ARUSHA

MAPOKEZI ya Mwenge wa Uhuru yanayotarajiwa kufanyika Julai 9, 2026 katika Jiji la Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modest Mkude, amezindua rasmi Jukwaa la Vijana (Youth Platform) la Wilaya ya Arusha, akisisitiza kuwa litakuwa chachu ya kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na uongozi.

Uzinduzi wa jukwaa hilo, uliofanyika Julai 6, 2026, ni sehemu ya maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru na utekelezaji wa jitihada za Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Wizara ya Maendeleo ya Vijana za kuwajengea vijana uwezo wa kutumia fursa zilizopo kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkude alisema jukwaa hilo litakuwa kiunganishi muhimu kati ya vijana na taasisi mbalimbali zinazotoa fursa za ajira, ujasiriamali na maendeleo, huku akiwataka vijana kulitumia kujifunza, kujenga mitandao na kuongeza uwezo wa kujitegemea kiuchumi.

Alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kutoka Ofisi ya Rais na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Uraia, Uzalendo na Uratibu wa Mwenge wa Uhuru, Suleiman Mvunye, aliwataka vijana kuishi kwa kuzingatia misingi ya Mwenge wa Uhuru inayohimiza umoja, uzalendo, uwajibikaji na ushiriki katika maendeleo ya taifa.

Mvunye aliwahimiza vijana kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia maadili mema, kulinda amani ya nchi na kuendelea kuenzi kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru 2026 isemayo, "Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo."

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Lipes Kayombo, alisema jiji hilo lina fursa nyingi za kiuchumi ambazo vijana wanapaswa kuzitumia ili kujikwamua kiuchumi.

Alieleza kuwa Halmashauri ya Jiji inaendelea kuratibu programu mbalimbali za kuwawezesha vijana, ikiwemo utoaji wa mikopo ya asilimia nne isiyo na riba kwa makundi ya vijana ili kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza miradi ya uzalishaji mali.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Jacob Julius Rombo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Eliakimu Mnzava, viongozi wa Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kupokelewa rasmi katika Jiji la Arusha Julai 9, 2026 ukitokea Mkoa wa Kilimanjaro, ukiendelea kuhamasisha uzalendo, mshikamano, uwajibikaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.








Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post