CCM YALIA NA MFANYABIASHARA ARUSHA, YAMTUHUMU KUVUNJA TAWI NA KUKATA MTI WA KIHISTORIA
Na Joseph Ngilisho|ARUSHA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kati jijini Arusha kimeingia katika mgogoro na mfanyabiashara mmoja, kikimtuhumu kuvunja Tawi Na. 3 la chama hicho lililozinduliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na kuzungushia eneo hilo uzio wa mabati na kukata mti mkubwa wa kihistoria uliokuwa ndani ya eneo la tawi hilo.
Tawi hilo, lililopo Mtaa wa Bondeni, Soko Kuu, Kata ya Kati jijini Arusha, lilizinduliwa na Dk. Nchimbi wakati akiwa Katibu Mkuu wa CCM, ambapo pia alichangia shilingi milioni mbili kwa ajili ya kuboresha shughuli za tawi hilo baada ya kujiridhisha kuwa eneo hilo ni mali halali ya CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kati, Kirenga Swai, alisema mfanyabiashara huyo amekuwa akiingilia eneo la chama kwa muda mrefu, akidai kuwa hata mwaka jana aliweka uzio wa mabati na kuacha sehemu ndogo ya tawi hilo huku akiingia ndani ya eneo linalomilikiwa na CCM.
Swai alisema tukio la hivi karibuni lilifanyika usiku wa kuamkia Jumamosi baada ya Ijumaa, ambapo mfanyabiashara huyo anadaiwa kukata mti huo mkubwa wa kihistoria na kuzungushia eneo hilo uzio wa mabati kwa siri, jambo alilodai lililenga kukwepa usimamizi wa viongozi na mamlaka husika. Alisema kufanya shughuli hizo usiku ni kinyume cha taratibu na sheria, hivyo hatua za kisheria zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Aliongeza kuwa eneo hilo hutumiwa na wafanyabiashara wadogo wa kahawa kufanyia biashara zao kupitia tawi la CCM, hivyo hatua ya kuvunja tawi, kukata mti huo na kuzungushia uzio imeathiri shughuli za chama pamoja na wananchi wanaotegemea eneo hilo kujipatia kipato.
Kwa mujibu wa Swai, mti uliokatwa ulikuwa na historia ya zaidi ya miaka 70 na ulikuwa sehemu ya urithi wa eneo hilo. Alidai mfanyabiashara huyo aliukata bila kibali kutoka mamlaka husika, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Aidha, alisema baada ya kupokea malalamiko hayo, maofisa wa Idara ya Mipango Miji ya Jiji la Arusha walifika eneo la tukio na kuweka alama ya "X" pamoja na maandishi ya "ONDOA", wakimtaka mfanyabiashara huyo kuondoa uzio wa mabati unaodaiwa kuingia katika eneo la CCM.
Naye Diwani wa Kata ya Kati, Mheshimiwa Abdulrasul Tojo , alisema hakushirikishwa wala kupewa taarifa kuhusu kukatwa kwa mti huo au ujenzi wa uzio wa mabati. Alisema si mara ya kwanza kwa mfanyabiashara huyo kufanya jaribio la kuingilia eneo hilo, akidai kuwa hata tukio la awali hakutoa ushirikiano kwa viongozi waliotaka kufuatilia suala hilo.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Kati, Charles Mollel, alikanusha kutoa kibali cha kukatwa kwa mti huo, akieleza kuwa kibali alichotoa kilihusu kupogoa matawi ya mti na si kuukata kabisa.
Mollel alisema atamwandikia mfanyabiashara huyo barua ya wito ili afike ofisini kutoa maelezo kuhusu hatua alizochukua, huku akisisitiza kuwa suala hilo litafuatiliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za mamlaka husika.
Ends..










Post a Comment