LUKUMAY AWAPA POLE FAMILIA YA MWENYEKITI WA CCM KIRANYI, AHIMIZA KUWATHAMINI WAZAZI WAKIWA HAI
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ametoa salamu za pole kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kiranyi, James Kivuyo, pamoja na familia nzima kufuatia kifo cha mama yao mzazi, Damari Kivuyo(99), akisema msiba huo ni pigo kubwa kwa familia na jamii iliyomfahamu marehemu.
Akizungumza wakati wa ibada na shughuli za mazishi, Dkt. Lukumay alisema marehemu Damari Kivuyo alikuwa mwanamke mwenye upendo na mchango mkubwa katika jamii, huku akimtaja James Kivuyo kuwa kiongozi aliyekuwa akilelewa na kuungwa mkono na mama mwenye maadili mema.
Lukumay alisema kifo ni sehemu ya maisha ambayo hakuna binadamu anayeweza kuizoea, akisisitiza kuwa maumivu ya kumpoteza mama mzazi ni makubwa kuliko ilivyo kwa misiba mingine.
"Hakuna mtu mwenye upendo wa kweli duniani anayelinganishwa na mama mzazi. Kwa wale ambao Mwenyezi Mungu bado amewajalia kuwa na mama zao, nawasihi wawatunze, wawaheshimu na kuwapa kila wanachohitaji, kwa sababu mama hana mbadala," alisema Lukumay.
Mbunge huyo aliipongeza familia ya marehemu kwa kujitoa kumhudumia na kumuuguza mama yao hadi mwisho wa maisha yake, akieleza kuwa hilo ni jambo la kujivunia na mfano wa kuigwa katika jamii.
Alisema msiba huo umeigusa familia, ndugu, marafiki na wananchi wa Kata ya Kiranyi, lakini akawahimiza wote kuendelea kumtegemea Mungu kwa kuwa ndiye mfariji wa kweli katika nyakati za majonzi.
Aidha, Lukumay aliwataka wananchi kuendelea kuishi kwa amani, upendo na mshikamano, wakitambua kuwa maisha ya mwanadamu hapa duniani ni mafupi na hakuna anayejua siku wala saa yake.
"Mama Damari amemaliza safari yake duniani. Sisi tuliobaki tujiulize tunaishi maisha ya namna gani na tunaacha alama gani kwa jamii. Matendo mema ndiyo yatakayobaki kutukumbusha baada ya kuondoka kwetu," alisema.
Alihitimisha kwa kuifariji familia ya Kivuyo na kuwaombea nguvu katika kipindi hicho kigumu, huku akisema ni Mungu pekee anayeweza kuponya majeraha ya mioyo ya wafiwa na kuwapa faraja ya kweli.















Post a Comment