KIWANJA CHA KISASA CHA MICHEZO CHA SH. BILIONI 2.5 CHAJENGWA LONGIDO, KULENGA MICHEZO YA AFCON 2027,KUIBUA VIPAJI ,MWENGE WA UHURU 2026 WAPONGEZA

Na Joseph Ngilisho | Longido

 



WILAYA ya Longido inatarajiwa kuwa kitovu kipya cha maendeleo ya michezo nchini baada ya kuanza ujenzi wa Longido Sports and Retreat Center, mradi wa kisasa wenye thamani ya Shilingi bilioni 2.5 unaolenga kuibua na kukuza vipaji vya watoto na vijana, sambamba na kujiandaa kupokea timu zitakazoweka kambi wakati wa fainali za AFCON 2027.

Mkurugenzi Mwanzilishi wa Sports Impact and Discipleship Development (SIDD) na Rabbit Stars Academy, Daniel Laizer, alisema mradi huo unaojengwa katika kijiji cha Oltepesi ,Olbomba utabadilisha taswira ya michezo katika Wilaya ya Longido kwa kuweka miundombinu ya kisasa itakayowawezesha watoto na vijana kukuza vipaji vyao katika mazingira salama na rafiki.

Laizer alitoa kauli hiyo leo Julai 5, 2026, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, kufuatia uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi huo katika Wilaya ya Longido, mkoani Arusha.

Alisema wazo la kuanzisha kituo hicho lilitokana na kutambua kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa miundombinu ya michezo nchini, jambo linalozuia vipaji vya vijana kukua na kuleta tija kwa jamii na taifa.

"Michezo si burudani pekee, bali ni afya, ajira na fursa ya maisha. Kupitia kituo hiki tunataka kuibua, kulea na kukuza vipaji vya watoto na vijana ili viweze kuwanufaisha wao binafsi na taifa kwa ujumla," alisema.

Alieleza kuwa maandalizi ya mradi yalianza Desemba 2024, huku ujenzi rasmi ukianza Juni 2025 baada ya kupatikana kwa ufadhili kutoka kwa wadau wa ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Laizer, mradi huo unagharimu Shilingi bilioni 2.5, huku hadi sasa ukiwa umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika kwa asilimia 100 ifikapo Juni 2027.

Alisema kituo hicho kitakuwa na uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu wenye viwango vinavyokidhi masharti ya kimataifa, uwanja wa mazoezi, vyumba vya kubadilishia nguo na jukwaa la watazamaji.

Pia kitakuwa na viwanja viwili vya mpira wa wavu vya mchanga, uwanja mkubwa wa mpira wa kikapu wenye viwanja vitatu kwa makundi tofauti ya umri, uwanja wa netiboli, hostel kwa ajili ya timu zitakazoweka kambi, jengo la utawala lenye ukumbi wa mikutano, sehemu za mafunzo, jiko, nyumba ya wageni, ofisi na huduma nyingine muhimu.

Laizer alisema utekelezaji wa mradi huo unaungwa mkono na shirika la Fellowship of Christian Athletes (FCA) kutoka Marekani, ambalo limekuwa mshirika mkuu katika kufadhili shughuli za ujenzi na programu zinazotumia michezo kujenga maadili na kuwawezesha vijana kutumia vipaji vyao kwa maendeleo.

Aliishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwa ushirikiano walioutoa tangu hatua za awali za mradi, ikiwemo kusaidia upatikanaji wa eneo la zaidi ya ekari 10 kupitia Idara ya Ardhi pamoja na ushirikiano wa Idara ya Michezo katika kuendesha Rabbit Stars Academy.

Aidha, alisema wanaendelea kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Arusha Regional Football Association (ARFA) kuhakikisha miundombinu inayojengwa inakidhi viwango vya kimataifa.

Alisema lengo lao ni kuona Longido Sports and Retreat Center ikitumika kama kambi ya maandalizi kwa angalau timu moja itakayoshiriki fainali za AFCON 2027 zitakazofanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda.

"Tunaamini Longido inaweza kuwa sehemu ya historia ya AFCON 2027. Tunaendelea kufanya mawasiliano na mamlaka husika ili kuhakikisha kituo hiki kinakidhi viwango vinavyohitajika na kuwa miongoni mwa maeneo yatakayopokea timu zitakazoshiriki mashindano hayo," alisema.

Akikagua mradi huo Kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa,Wazo Mwang'onda alimpongeza mwekezaji huyo kwa kuthubutu kufanya uwekezaji huo mkubwa Longido, kwa kutambua Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050 ikiwa imejikita katika uwekezaji kwenye sekta binafsi hususani katika michezo, ambayo kimsingi inatoa ajira nyingi duniani na kuwataka wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuwekeza nchini.

Hata hivyo amewataka wananchi kuendelea kulinda amani ya Tanzania, amani ambayo inasababisha wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji zinazoinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. 





Ends ..


Post a Comment

Previous Post Next Post