KILIO CHA MBUNGE LUKUMAY CHASIKIKA, MWENGE WA UHURU WATOA SIKU NNE KWA TARURA KUCHONGA BARABARA BWAWANI,KUONDOA VUMBI

KILIO CHA MBUNGE LUKUMAY CHASIKIKA, MWENGE WA UHURU WATOA SIKU NNE KWA TARURA KUCHONGA BARABARA BWAWANI,KUONDOA VUMBI

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

Hatimaye kilio cha Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, kuhusu ubovu wa barabara katika Kata ya Bwawani kimesikika baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazi Mwang'onda, kuagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kuhakikisha barabara hiyo inachongwa na mashimo yanaondolewa ili kupunguza kero kwa wananchi.

Maagizo hayo yalitolewa wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru baada ya wananchi na Mbunge huyo kueleza changamoto wanazozipata kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

Akitoa maelekezo, Mwang'onda alisema Mwenge wa Uhuru umesikia kilio cha mbunge. na wananchi na umejiridhisha kuwa barabara hiyo ipo katika hali mbaya, hivyo hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa.

"Kilio cha wananchi kimesikika. Barabara hii itaanza kurekebishwa muda si mrefu. TARURA hakikisheni ndani ya siku mbili, tatu au nne mnaichonga barabara hii na kuondoa mashimo ili wananchi waweze kupita kwa urahisi wakati taratibu za ukarabati zaidi zikiendelea," alisema Mwang'onda.

Aliongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kuwajali wananchi na kutatua changamoto zao za maendeleo, ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara.

Awali, akizungumza wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Dkt. Lukumay aliiomba Serikali kuingilia kati haraka na kuielekeza TARURA kutatua kero ya barabara hiyo, akieleza kuwa imekuwa chanzo cha usumbufu mkubwa kwa wananchi, hususan wakati wa masika kutokana na matope na wakati wa kiangazi kutokana na vumbi.

Mbunge huyo alisema uboreshaji wa barabara hiyo utarahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao, huduma za kijamii na shughuli nyingine za kiuchumi kwa wakazi wa Kata ya Bwawani na maeneo jirani.

Ends .

Post a Comment

Previous Post Next Post