Na Joseph Ngilisho | Arusha
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, amemkabidhi jukumu zito Kamishna mpya wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa, akimtaka kuimarisha nidhamu na uwajibikaji wa watumishi, kuboresha maslahi yao, kuongeza ufanisi wa utendaji pamoja na kusimamia kwa nguvu mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka ili kulinda hadhi ya taasisi hiyo.
Kijaji alitoa maelekezo hayo jijini Arusha leo Alhamis Julai 9,2026 wakati wa hafla ya kumvisha cheo na kumuapisha rasmi Mwishawa kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA,iliyofanyika makao Makuu ya TANAPA, akisema Serikali ina matarajio makubwa kwake kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika sekta ya uhifadhi.
Alisema uteuzi wa Mwishawa uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, ni ishara ya imani kubwa ambayo Serikali imeweka kwake kutokana na uadilifu, uzalendo, weledi na uwezo wake wa kuiongoza TANAPA katika kipindi ambacho sekta ya uhifadhi na utalii inaendelea kukua kwa kasi.
"Serikali ina matarajio makubwa kwamba utaiongoza TANAPA kwa uelewa, uadilifu, nidhamu na maono yatakayofanya taasisi hii kuendelea kuwa mfano bora wa uhifadhi barani Afrika na duniani," alisema Kijaji.
Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya uhifadhi na utalii kupitia ujenzi wa miundombinu, matumizi ya teknolojia za kisasa, kuimarisha mifumo ya usimamizi wa bioanuwai pamoja na kampeni za kimataifa za kuitangaza Tanzania kama kivutio kikuu cha utalii.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hizo zimeongeza idadi ya watalii, mapato ya utalii na uwekezaji katika hifadhi za taifa, hivyo kuifanya TANAPA kuwa na wajibu mkubwa zaidi wa kulinda rasilimali hizo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Akizungumza moja kwa moja na Kamishna mpya, Kijaji alisema askari na maafisa uhifadhi ndio nguzo kuu ya mafanikio ya TANAPA, hivyo wanapaswa kuongozwa kwa misingi ya nidhamu, uwajibikaji na uzalendo.
"Ufanisi wa TANAPA katika kupambana na ujangili, kudhibiti uvamizi wa hifadhi na kulinda bioanuwai unategemea askari na maafisa wenye maadili, weledi na uzalendo.
Hakikisha unajenga nidhamu isiyotetereka ndani ya taasisi," alisisitiza.
Aidha, alisema Serikali haitavumilia vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, utovu wa nidhamu wala matumizi mabaya ya mali za umma yanayoweza kuchafua taswira ya TANAPA na Serikali kwa ujumla.
Pia alimwelekeza Mwishawa kushughulikia changamoto za watumishi, akisema kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kuhusu ucheleweshaji wa stahiki na mazingira ya kazi.
"Serikali inatambua kuwa mtumishi mwenye motisha na anayefanya kazi katika mazingira bora ndiye msingi wa taasisi yenye mafanikio.
Hakikisha ustawi wa watumishi unapewa uzito unaostahili," alisema.
Kwa upande wake, Kamishna mpya wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Mwishawa, alisema anaipokea dhamana hiyo kwa unyenyekevu mkubwa na kuahidi kuiongoza taasisi hiyo kwa uwajibikaji, uadilifu na weledi huku akiahidi kuongeza mapato ya Serikali kupitia utalii, kuimarisha ulinzi wa maliasili na kuboresha maslahi ya watumishi.
"Ninaipokea dhamana hii kwa unyenyekevu mkubwa. Nitaitekeleza kwa uzalendo, uwadilifu, weledi na kwa kushirikiana na watumishi wenzangu ili kuhakikisha TANAPA inaendelea kutimiza wajibu wake kwa taifa," alisema.
Alisema katika kipindi cha uongozi wake atajikita katika kuboresha mazingira ya kazi na ustawi wa watumishi, kuongeza ukusanyaji wa mapato, kuimarisha ulinzi wa maliasili dhidi ya uhalifu, kuboresha miundombinu ya utalii ikiwemo barabara na viwanja vya ndege ndani ya hifadhi, pamoja na kuimarisha ushirikiano na wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi.
Mwishawa alisema mafanikio ya TANAPA yatategemea mshikamano wa watumishi wote na kuwataka maafisa pamoja na askari wa uhifadhi kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku wakizingatia maadili ya uwajibikaji, ushirikiano, ubunifu na ubora katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara, alisema uteuzi wa Mwishawa unaonyesha imani kubwa ya Serikali kutokana na uzoefu wake mpana ndani ya TANAPA, ambako amepitia ngazi mbalimbali za uongozi hadi kufikia nafasi ya Naibu Kamishna wa Uhifadhi.
"Kamishna Mwishawa ni zao la TANAPA. Amefanya kazi katika ngazi mbalimbali za shirika hili, ikiwemo kuwa Kamanda wa Kanda na baadaye Naibu Kamishna. Analifahamu vyema shirika, watumishi wake na mazingira ya kazi, jambo linalotupa imani kuwa ataliongoza kwa mafanikio makubwa zaidi," alisema Waitara.
Aliwataka maafisa, askari na watumishi wote wa TANAPA kumpa ushirikiano wa dhati Kamishna huyo mpya, akisisitiza kuwa mafanikio ya shirika yanategemea mshikamano na kufanya kazi kama timu moja.
"Ninawaomba wote mumuunge mkono. Mabadiliko yoyote atakayofanya katika utendaji yaeleweke kuwa yanalenga kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa shirika. Ushirikiano ni msingi wa mafanikio ya taasisi yoyote," alisema.
Aidha, Waitara alisema Bodi ya Wadhamini itaendelea kumpa ushauri na mwongozo Kamishna huyo mpya ili kuhakikisha TANAPA inaendelea kufikia malengo yake ya uhifadhi na kuchangia zaidi maendeleo ya sekta ya utalii na uchumi wa taifa.
Katika hafla hiyo, Waziri Kijaji pia alimpongeza aliyekuwa Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Musa Nasoro Kuji, kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha uhifadhi na kukuza sekta ya utalii nchini, huku akimtakia mafanikio katika hatua nyingine za maisha yake.
***ENDS***




Post a Comment