DAKTARI BINGWA KUTOKA UJERUMANI AAHIDI KUIJENGEA UWEZO TANZANIA KUDHIBITI MAGONJWA YA KINYWA NA MENO
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
DAKTARI bingwa wa afya ya kinywa na meno kutoka Ujerumani, Dkt. Ursula Suessbier, ameahidi kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani katika kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno baada ya kubaini kuwa changamoto za magonjwa ya kinywa na meno nchini bado ni kubwa na zinahitaji ushirikiano wa karibu wa kimataifa katika tiba, kinga na mafunzo ya wataalamu.
Dkt. Suessbier alitoa ahadi hiyo leo Julai 24,2026 alipokuwa akihitimisha kambi maalumu ya siku mbili ya matibabu ya afya ya kinywa na meno katika Hospitali ya Selian-Ngaramtoni, iliyokuwa hitimisho la ziara ya siku saba ya madaktari bingwa wa afya ya kinywa na meno katika Jimbo la Arumeru Magharibi.
Ziara hiyo iliwakutanisha madaktari bingwa kutoka Ujerumani na wenzao wa Tanzania, wakiwemo wataalamu kutoka Halmashauri ya Arusha na Hospitali ya Selian-Ngaramtoni, ambapo walitoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa mamia ya wananchi, walifanya uchunguzi wa afya ya meno katika shule za msingi na sekondari, na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu kwa lengo la kuimarisha huduma za afya ya kinywa na meno nchini.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa shughuli hizo, Dkt. Suessbier alisema uzoefu alioupata Arumeru umeonyesha kuwa Tanzania inahitaji kuwekeza zaidi katika huduma za kinga na kuongeza ushirikiano wa kimataifa ili kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani.
Alisema uchunguzi uliofanywa shuleni umebaini kuwa watoto wengi wana meno imara, ingawa baadhi yao walikuwa na matatizo ya kuoza kwa meno kwa kiwango kidogo. Hata hivyo, alisema hali ilikuwa tofauti kwa watu wazima waliotibiwa katika Hospitali ya Selian-Ngaramtoni.
Kwa mujibu wa Dkt. Suessbier, wagonjwa wengi watu wazima walikuwa na uchafu mgumu ulioganda kwenye meno (calculus) pamoja na magonjwa ya fizi (periodontal diseases), matatizo ambayo yanaweza kusababisha meno kulegea na hatimaye kung'oka ikiwa hayatatibiwa mapema.
"Tuliona changamoto kubwa si kuoza kwa meno pekee, bali magonjwa ya fizi. Haya yanaweza kuzuilika kwa kusafisha meno mara moja au mbili kwa mwaka, jambo ambalo ni la kawaida nchini Ujerumani. Tukiboresha huduma za kinga hapa Tanzania, afya ya kinywa na meno itaimarika kwa kiwango kikubwa," alisema.
Alieleza kuwa moja ya malengo makuu ya ushirikiano huo ni kuanzisha programu ya kubadilishana utaalamu kati ya Tanzania na Ujerumani, itakayowezesha madaktari, wasaidizi wa madaktari wa meno na wataalamu wa usafi wa meno kupata mafunzo ya kisasa na kuboresha huduma wanazozitoa kwa wananchi.
Dkt. Suessbier alisema taasisi ya Dental Global itaendelea kushirikiana na wadau wa afya nchini kwa kuwaleta wataalamu kutoka Berlin kutoa mafunzo kwa wenzao wa Tanzania, huku ikiendeleza pia programu za elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa usafi wa meno na kinga dhidi ya magonjwa ya kinywa.
Alisisitiza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani, kuboresha huduma za kinga na matibabu, na kupunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa magonjwa ya afya ya kinywa na meno nchini.
Ends..




Post a Comment